Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa imetangaza kuwa itafunga rasmi ofisi yake nchini Burkina Faso ifikapo tarehe 30 Novemba 2026, miezi mitatu baada ya mamlaka ya kijeshi ya nchi hiyo kusitisha shughuli zake kwa muda usiojulikana.
Hatua hiyo inahitimisha uwepo wa miaka mitano wa ofisi hiyo katika taifa hilo la Afrika Magharibi, ambako ilishirikiana na taasisi za serikali na kutoa mafunzo kwa maelfu ya maafisa wa usalama wakati nchi ikikabiliwa na kuzorota kwa hali ya usalama.
Akizungumza Alhamisi, Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu, Volker Türk, alisema juhudi za muda mrefu za kutafuta suluhu na mamlaka ya Burkina Faso hazikufanikiwa.
“Ninasikitishwa sana na uamuzi wa mamlaka ya Burkina Faso wa kusitisha shughuli zetu nchini kwa muda usiojulikana. Pia, mazungumzo ya kina yaliyofanyika tangu wakati huo hayakuweza kutatua suala hili. Hali hiyo imeathiri moja kwa moja uwezo wetu wa kutekeleza wajibu wetu na imenilazimu kufanya uamuzi wa kufunga ofisi yetu nchini humo,” alisema Türk.
Serikali ya Burkina Faso haijatoa tamko
Hadi sasa, serikali ya Burkina Faso haijatoa kauli rasmi kuhusu uamuzi wa Umoja wa Mataifa wa kufunga ofisi hiyo.
Shughuli za ofisi hiyo zilisitishwa miezi mitatu iliyopita baada ya Umoja wa Mataifa kutoa taarifa kwa vyombo vya habari ukitaka serikali ya nchi hio kulinda na kuheshimu nafasi ya wananchi kutumia haki zao za kiraia, ikiwemo uhuru wa kujieleza na kushiriki katika shughuli za kijamii na kisiasa.
Hata hivyo, Türk alisema kuwa licha ya kufungwa kwa ofisi hiyo, Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa itaendelea kushirikiana na Burkina Faso kuhusu masuala ya haki za binadamu kutoka nje ya nchi.
“Licha ya kufungwa kwa ofisi hii, mimi na Ofisi yangu tunaendelea kujizatiti kuunga mkono na kushirikiana na serikali, taasisi za kitaifa, asasi za kiraia na wadau wengine katika masuala ya haki za binadamu,” alisema.
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu ilifungua ofisi yake nchini Burkina Faso mwezi Oktoba 2021, wakati taifa hilo lilikuwa linakabiliwa na kuzorota kwa kasi kwa hali ya usalama kutokana na mashambulizi ya makundi ya kigaidi.















