Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Hakan Fidan na mwenzake kutoka Jordan Ayman Safadi wamekuwa na mazungumzo ya simu, wakijadiliana kuhusu hali halisi inayoendelea Syria na Gaza, kulingana na vyanzo vya kidiplomasia vya Uturuki.
Wawili hao, pia walipata fursa ya kujadiliana uhusiano wa nchi hizo mbili pamoja na masuala ya kikanda, siku ya Jumatatu.
Safadi aliitembelea Ankara mnamo tarehe 6 Januari na kuwa na mkutano wa pamoja na wanahabari akiwa na Fidan.
Safadi aligusia umuhimu wa kukuza ushirikiano na uratibu kati ya nchi hizo wakati wa mkutano huo ili kuweza kutatua changamoto za kikanda, ikiwemo mchakato wa ujenzi mpya wa Syria na urejeshwaji wa utulivu katika eneo la Mashariki ya Kati.
Safadi pia alikazia jitihada za Jordan kuunga mkono watu wa Palestina katika mapambano yao ya kuwa na dola yao huru kwa kuzingatia mipaka ya 1967.