Mazungumzo kati ya Israeli na Palestina, yaliyosimamiwa baina ya Marekani, Qatar na Misri, hadi sasa yameshindwa kupata makubaliano ya usitishaji wa vita vya kudumu vya Israeli dhidi ya Gaza ya Palestina.
Katika mazungumzo ya simu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken siku ya Ijumaa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Hakan Fidan aligusia pendekezo la hivi karibuni la lililoibuka katika maridhiano kati ya kikundi cha Kipalestina cha Hamas na Israeli, kulingana na vyanzo vya kidiplomasia.
Hapo awali, Rais wa Marekani Joe Biden alisema kuwa Israeli imewasilisha kwa Hamas, mpango wa awamu tatu ambao utamaliza uhasama katika eneo lililozingirwa la Gaza na kuwaachilia mateka wanaoendelea kuzuiliwa katika eneo la pwani.
"Ni wakati wa kuanza hatua hii mpya, mateka warudi nyumbani, ili Israeli iwe salama, ili mateso yakome. Ni wakati wa vita hivi kumalizika, kwa siku inayofuata kuanza," rais alisema katika hotuba yake kutoka Ikulu.
Tel Aviv imeendelea na mashambulizi yake licha ya azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linalotaka maridhiano.
Miezi nane ya vita
Israeli imeua zaidi ya Wapalestina 36,000 katika eneo la Gaza toka kutokea shambulizi la mpakani la Hamas la Oktoba 7, 2023 lililoua watu 1,200 na kuwageuza watu 250 mateka.
Takriban mateka 105 waliachiliwa kama sehemu ya mapatano mafupi mwezi Novemba kwa kubadilishana na wafungwa 240 wa Kipalestina.
Watu wengine 125 bado wanashikiliwa mateka, wengi wakiaminika kuwa wamepoteza maisha kufuatia mashambulizi ya angani ya Israeli.
Takriban miezi minane ya vita vya Israeli, maeneo makubwa ya Gaza yamegeuka kuwa magofu huku kukiwa na vizingiti vya upatikanaji wa chakula, maji safi na dawa.
Israeli inashutumiwa kwa "mauaji ya halaiki" katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ), ambayo katika uamuzi wake wa hivi karibuni, iliiamuru Tel Aviv kusitisha mara moja operesheni yake huko Rafah, mji ulioko kusini mwa Gaza ambako zaidi ya Wapalestina milioni moja waliokimbia makazi yao walikuwa wametafuta hifadhi.