Tayari Uturuki imekuwa ikitekeleza njia thabiti za nishati na mkakati wa utofautishaji wa vyanzo na ajenda kabambe ya kuelekea matumizi ya nishati safi," Fidan alisema. /Picha: AA  

Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki amehimiza hatua za usalama wa nyuklia na kutokomeza nyuklia katika kanda wakati wa Mkutano wa kwanza wa Nishati ya Nyuklia huko Brussels, akielezea wasiwasi wake juu ya hali katika Kiwanda cha Nguvu za Nyuklia cha Zaporizhzhia.

Akihutubia mkutano huo ulioandaliwa na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) na Ubelgiji mjini Brussels siku ya Alhamisi, Hakan Fidan Alhamisi alisisitiza umuhimu wa kuimarishwa kwa hatua za usalama za matumizi ya nyuklia na kusisitiza dhamira ya Uturuki katika juhudi za kikanda za kukomesha nyuklia.

"Mkutano huo unajumuisha hatua za mageuzi kuhusu mustakabali wa nishati ya nyuklia," alisema.

Akitoa msisitizo kuhusu mkakati kabambe wa nishati wa Uturuki, Fidan alielezea hatua ya taifa kuelekea nishati safi na mchango wake mkubwa katika usalama wa nishati na kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Nishati mseto

"Tayari, Uturuki imekuwa ikitekeleza njia thabiti za nishati na mkakati wa utofautishaji wa vyanzo na ajenda kabambe ya kuelekea nishati safi," alisema.

Akiangazia juhudi za Uturuki katika nyanja ya kiraia ya nyuklia, Fidan alisema: "Kiwanda cha Nishati ya Nyuklia cha Akkuyu ni mradi wetu mkuu. Pindi kitakapofanya kazi kikamilifu, kitatosheleza asilimia 10 ya mahitaji yetu ya umeme."

Akizungumzia hali ya Kiwanda cha Nguvu za Nyuklia cha Zaporizhzhia, Fidan alionesha wasiwasi wake mkubwa, akitaja uzoefu wa Uturuki na maafa ya Chornobyl.

Akirejelea maafa ya Chornobyl, alisema: "Hatuwezi kuruhusu kutokea kwa mengine. Uturuki imechukua hatua kadhaa kuepusha tukio la kutisha katika jiji la Zaporizhzhia kusini mashariki mwa Ukraine."

Hatari ya matumizi ya Nyuklia

Fidan alihakikishia utayari wa Ankara katika mipango inayolenga kuepusha maafa yanayoweza kutokea katika Kiwanda cha Nishati ya Nyuklia cha Zaporizhzhia na kuunga mkono juhudi za mkurugenzi mkuu wa IAEA katika kushughulikia suala hilo.

Akilaani matumizi ya silaha za nyuklia, Hakan Fidan anasema kuwa kauli zinazotawala "silaha za nyuklia huweka kivuli kwenye harakati zetu za pamoja za mustakabali safi ulio salama na wenye hekima kwenye matumizi ya nishati."

Aligusia eneo la Mashariki ya Kati kama "eneo lenye hali mbaya zaidi" katika muktadha huu, akitolea mfano mzozo unaoendelea huko Gaza na maoni ya maafisa wa Israeli juu ya silaha za nyuklia.

"Wakati mauaji ya Gaza yanaendelea, maelezo ya maafisa wa Israeli kuhusu silaha za nyuklia hayawezi kupuuzwa kwani yanaonesha hali ya kutojali," alisema.

"Hivyo basi, Uturuki inasisitiza wito wake wa kuondoa nyuklia katika eneo hilo ili kuepusha uwezekano wa mashindano ya silaha za nyuklia," aliongeza.

Fidan aliishukuru Ubelgiji na IAEA kwa kuandaa mkutano huo, kwa kutambua nafasi yake katika kuandaa mustakabali wa nishati ya nyuklia.

TRT Afrika