Uturuki imemteua mwanamke katika ngazi ya Admiral kwa mara ya kwanza katika historia ya Jeshi la Wanamaji la Uturuki, kufuatia mkutano wa Baraza Kuu la Kijeshi, siku ya Alhamisi.
Kanali mtendaji Gokcen Firat atakuwa Rear Admiral (Lower Half) RDML katika Kikosi cha Wanamaji cha Uturuki.
Uamuzi huo umejiri baada ya mkutano wa faragha ulioongozwa na Rais Recep Tayyip Erdogan.
Mkutano huo hutumika kama jukwaa la kuzindua ajenda ya kijeshi ya Uturuki na kwa kawaida hushughulikia masuala kama vile kupandisha vyeo, kuachishwa kazi na maamuzi mengine ya utendakazi.
Mkuu mpya wa Jeshi wa Uturuki
Miongoni mwa uteuzi uliofanywa ni wa Jenerali Metin Gurak kuwa Mkuu mpya wa majeshi ya Uturuki huku kukiwa na msururu wa maamuzi yaliyotangazwa baada ya mkutano wa Baraza Kuu la Kijeshi Alhamisi.
Gurak amehudumu kama kamanda wa Jeshi la pili tangu 2021.
Selcuk Bayraktaroglu, naibu mkuu wa majeshi, ndiye kamanda mpya wa Vikosi vya Ardhi, akichukua nafasi ya Musa Avsever, kulingana na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Uturuki.
Aidha, Jenerali Ziya Cemal Kadioglu aliteuliwa kuwa kamanda mpya wa Jeshi la Wanahewa kufuatia kustaafu kwa Atilla Gulan.
Jumla ya majenerali 32 na ma Admirali wanapandishwa vyeo vinavyofuata na Makanali 63 kupandishwa hadi Jenerali au Admirali kuanzia Agosti 30.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Idadi ya Majenerali na Maadmirali katika Jeshi la Uturuki itaongezeka kutoka 266 hadi 286.