Mbali na Uturuki, Jamhuri ya Kituruki ya Kupro ya Kaskazini (TRNC) pia imetangaza siku tatu za maombolezi ya kitaifa kwa waathirika wa shambulio la anga la Israeli katika hospitali moja huko Gaza. / Picha: AA

Uturuki imeanza maombolezi rasmi ya kitaifa ya siku tatu kuonyesha mshikamano na Palestina kufuatia shambulio la anga la Israel dhidi ya hospitali ya Al Ahli Arab huko Gaza ambalo liliua watu wasiopungua 500.

Baada ya Uturuki na Misri, Jamhuri ya Kituruki ya Kupro ya Kaskazini (TRNC) pia ilitangaza siku tatu za maombolezi ya kitaifa siku ya Alhamisi kwa ajili ya waathiriwa wa shambulio la anga la Israeli kwenye hospitali huko Gaza.

"Kama Uturuki, tunahisi mateso makubwa ya ndugu na dada zetu wa Palestina kwenye nyoyo zetu," Rais Recep Tayyip Erdogan alisema kwenye mtandao wa X akitangaza amri ya rais, siku ya Jumatano.

"Kama njia ya kuheshimu maelfu ya washuhuda wetu, ambao wengi wao ni watoto na raia wasiokuwa na hatia, siku tatu za maombolezI ya kitaifa zinatangazwa katika nchi yetu," amesema Rais Erdogan akiwakumbuka zaidi ya Wapalestina 3,500 ambao wameuawa kwenye mashambulio ya Israeli tangu Oktoba 7.

Hapo awali, Bunge la Uturuki lililaani vikali mashambulizi ya Israeli dhidi ya hospitali katika taarifa ya pamoja na kusisitiza kwamba kusambulia maeneo ya kutoa huduma za afya ni kinyume na sheria za vita.

Shambulio hilo la hospitali limelaaniwa vikali na Uturuki, huku Erdogan akitoa wito kwa watu wote kuchukua hatua za kukomesha "ukatili usio na kifani wa Israeli kule Gaza".

"Kuvamia hospitali yenye wanawake, watoto, na raia wasio na hatia ni mfano wa hivi karibuni wa mashambulizi ya Israeli bila maadili ya msingi ya kibinadamu," Erdogan alisema kwenye mtandao wa X kufuatia shambulio hilo.

"Kulipua hospitali kwa mabomu ni uhalifu mkubwa. Kuuwa watu ambao wanapokea matibabu ni uchungu mkubwa. Kulenga raia ni kutumia mbinu za ugaidi, kwa wazi na rahisi, " Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Uturuki Fahrettin Altun pia alisema katika taarifa kupitia X.

Wakati huo huo, baraza la mawaziri la Jamhuri ya Kituruki ya Kupro ya Kaskazini (TRNC) lilitangaza kipindi cha maombolezi kuanzia Oktoba 19-21 kutokana na vifo na majeraha ya mamia ya watu kufuatia mashambulizi ya hospitali moja huko Gaza, siku ya Jumanne.

TRT World