Somalia na uturuki waliendeleza urafiki wao wa karibu mwaka 2011 baada ya Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan kufanya ziara ya kihistoria nchini humo. / Picha: AA

Waziri wa Mambo ya Nje wa Somalia Ahmed Moallim Fiqi amekutana na Mesut Ozcan, mkurugenzi wa Chuo cha Kidiplomasia cha Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki, katika mji mkuu Mogadishu.

Mwishoni mwa Jumatatu, pande hizo mbili zilijadili kuimarisha ushirikiano katika maeneo muhimu ya mafunzo ya kidiplomasia na kupanua wigo wa maarifa kwa wanadiplomasia.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Somalia baada ya mkutano huo ilisema majadiliano hayo pia yalijikita katika kuimarisha uhusiano kati ya chuo cha Uturuki na Taasisi ya Kidiplomasia ya Somalia, kwa lengo la "kuinua ushirikiano na kukuza kubadilishana uzoefu na mazoea bora."

Ilisema Fiqi alionyesha shukrani kubwa kwa Uturuki kwa msaada wake thabiti kwa Somalia.

Ankara imetoa mafunzo kwa zaidi ya wanadiplomasia 80 wa Somalia katika kipindi cha miaka 15 iliyopita, kulingana na taarifa ya wizara hiyo.

Mahusiano ya karibu

Somalia na Uturuki zilikuza urafiki wao wa karibu mwaka 2011 baada ya Rais wa Uturuki (Waziri Mkuu wa wakati huo) Recep Tayyip Erdogan kufanya ziara ya kihistoria nchini humo - kiongozi wa kwanza asiye Mwafrika kufanya hivyo katika zaidi ya miaka 20.

Uturuki ina uhusiano mkubwa wa kihistoria na Somalia kwa kanuni ya mahusiano ya "kushinda na kushinda", ikiwa ni pamoja na zaidi ya miradi 150 ya misaada ya maendeleo iliyofanywa na Shirika la Ushirikiano na Uratibu la Uturuki (TIKA) tangu 2011.

Uturuki pia ina ubalozi wake mkubwa zaidi barani Afrika huko Mogadishu na ilijenga kituo chake kikubwa zaidi cha kijeshi cha ng'ambo huko ili kutoa mafunzo kwa Jeshi la Kitaifa la Somalia.

TRT World