Wanachama katika mkataba wa nafaka wa Bahari Nyeusi wanakaribia makubaliano mapya baada ya siku mbili za mazungumzo jijini Istanbul kati ya maafisa wa Ukraine, Urusi, Uturuki na Umoja wa Mataifa, UN.
“Tunaelekea kwenye makubaliano ya kurefusha mkataba wa nafaka," Waziri wa Ulinzi wa Uturuki Hulusi Akar alisema katika taarifa iliyotolewa na Wizara hiyo siku ya Ijumaa.
Pande hizo zilikutana jijini Istanbul Mei 10-11 kwa ajili ya mazungumzo ya kuongeza muda wa makubaliano hayo, ambayo yanatarajiwa kukamilika wiki ijayo.
Ikulu ya Kremlin ilisema mapema Alhamisi kwamba rais wa Urusi Vladimir Putin anaweza kuzungumza na rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan kuhusu kurefushwa kwa makubaliano hayo, lakini bado hakukuwa na mipango kama hiyo.
Uturuki na Umoja wa Mataifa, UN, walipitisha makubaliano mwezi Julai mwaka jana ili kusaidia kukabiliana na mzozo wa chakula duniani ambao umezidishwa na vita vya Moscow nchini Ukraine.
Moscow inatafuta dhamana
Mkataba huo unaruhusu mauzo ya nafaka kutoka Ukraine kupitia bahari nyeusi. Hii inasaidia kupunguza uhaba na kupunguza kupanda kwa bei ya nafaka , hali ambayo ilisababishwa na mashambulizi ya Urusi dhidi ya Ukraine.
Kufikia sasa, zaidi ya tani milioni 30 za nafaka zilisafirishwa kwa wale wanaohitaji chini ya mpango huo.
Lakini Urusi haijajitolea kufanya upya kwa mara ya tatu kabla ya mkataba huo kuisha Mei 18.
Moscow inadai kuhakikisha kwamba madai yake, ikiwa ni pamoja na kuondolewa kwa vikwazo kwa mauzo yake ya nafaka na mbolea nje ya nchi, yanatimizwa kwa muda uliowekwa ili kufanya upya mpango huo.