Wasafiri hao walikaribishwa kwa chai na vitafunio katika eneo la VIP. / Photo: AA

Uhamisho wa raia wa Uturuki na Jamhuri ya Uturuki ya Kupro ya Kaskazini (TRNC) kutoka Gaza umeendelea katikati ya mashambulizi ya Israeli katika eneo la Palestina.

Katika operesheni iliyofanywa kupitia ushirikiano wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki na Mamlaka ya Usimamizi wa Maafa na Dharura (AFAD), kundi la watu 100 waliletwa Uwanja wa ndege wa Istanbul kupitia ndege ya Shirika la Ndege la Uturuki kutoka Cairo, Jumatano.

Maafisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na AFAD walikaribisha kundi hilo, ikiwa ni pamoja na walemavu, wazee, wanawake na watoto, ambao walikuwa wameingia Misri kupitia kivukio cha Rafah.

Mmoja wa watu waliohamishwa, Abdullah Coskun, alionyesha furaha yake alipofika Uturuki.

"Namshukuru Mungu nimejumuika tena na familia yangu. Safari yetu kutoka huko kufika hapa ilikuwa ngumu sana, " alisema Coskun, ambaye alidhani hataweza kuona familia yake tena kwa sababu ya mashambulio ya kibaguzi ya Israeli.

Baada ya ukaguzi wa hati za kusafiria, baadhi ya waliookolewa waliondoka uwanja wa ndege peke yao, huku raia wa Jamhuri ya Uturuki ya Kupro ya Kaskazini (TRNC) na wale wanaoishi katika miji mingine wakipelekwa hoteli kwa mabasi yaliyotolewa na shirika la AFAD.

Kupitia shughuli za uokoaji zilizopangwa, takriban raia 350 wa Uturuki na Jamhuri ya Uturuki ya Kupro ya Kaskazini (TRNC) wamerudishwa hadi sasa, na uokoaji kutoka Gaza utaendelea.

TRT World