Uturuki ina nia ya kuendeleza jitihada za upatanishi kuhusu Ukraine, alisema Fidan. / Picha: AA  

Uhusiano kati ya Moscow na Ankara "unaendelea vizuri mno", Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Hakan Fidan amesema wakati wa kikao chake na Rais wa Urusi Vladimir Putin mjini Moscow.

“Zipo hatua za kuchukua katika biashara,” alisema Fidan siku ya Jumanne, kulingana na vyanzo vya kidiplomasia vya Uturuki.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Hakan Fidan alipokelewa na Rais wa Urusi Vladimir Putin katika Ikulu ya Kremlin, ambapo alihudhuria kikao cha BRICS.

"Uturuki imeazimia kuendeleza jitihada zote za upatanishi katika suala la Ukraine", Fidan alisema.

"Kuhusu Syria, tunafanya kila linalowezekana kuendeleza sera ya amani, ambayo nyinyi kama viongozi wawili (Putin na Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan), mmeipa kipaumbele,” aliongeza.

Aliongeza kuwa alipata fursa ya kujadili yote hayo wakati wa mazungumzo mjini Moscow.

Mchango wa Uturuki katika utatuzi wa migogoro

Rais wa Urusi Vladimir Putin alikaribisha nia ya Uturuki katika ukanda wa BRICS.

"Tunaiunga mkono Uturuki ndani ya BRICS. Bila shaka, tutaunga mkono kwa dhati nia hii ya kuwa pamoja na nchi za jumuiya hii, kuwa pamoja, karibu zaidi, kutatua matatizo ya pamoja,” Putin alisema wakati wa kikao na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Hakan Fidan mjini Moscow.

Akihimiza muingiliano wa kina zaidi kati ya nchi za BRICS, Putin alisema ipo haja ya kupitia matendo yao katika nyanja ya kimataifa, katika suala la kuhakikisha usalama na mwingiliano wa kiuchumi.

Hapo awali, nchi za BRICS zilihusisha Brazil, Russia, India, China, and South Africa, huku Iran , Misri, Ethiopia na Umoja wa Nchi za Falme za Kiarabu zikijiunga mwezi Januari mwaka 2024.

Mkataba wa Nafaka katika Bahari Nyeusi

Pia Putin, alipongeza nia ya Ankara ya kusaidia kutatua vita kati ya Urusi na Ukraine vilivyoanza Februari 2022.

Putin aligusia nafasi ya Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan katika kuja na mpango Mkataba wa Nafaka wa Bahari Nyeusi wa mwaka 2022-2023 , katika kutatua tatizo la njaa duniani, na kumshukuru Fidan kwa kuunga mkono juhudi za upatanishi kati ya Moscow na Kiev.

Uturuki imejizolea sifa kutokana na uwezo wake kuzungumza na pande zote mbili, pamoja na mkataba wa nafaka na mpango wa kubadilishana wafungwa.

"Kwa pamoja, tumefanya jukumu muhimu sana katika kutatua mzozo wa Syria," Putin alisema kuhusu juhudi chini ya muundo wa Astana kuhimiza suluhu ya muda mrefu ndani ya Syria ambayo imekumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe.

"Nadhani ni vyema kuendeleza muundo wa Astana, kupambana na ugaidi na kufanya kila jitihada kuhakikisha kuwa hali ya kawaida inarejea," aliongeza.

“Tunashukuru sana mchango wa marafiki zetu Waturuki katika kutatua migogoro mbalimbali, ukiwemo ule wa Ukraine ,” aliongeza Putin.

Uhusiano wa nchi mbili

Kuhusu uhusiano wa Urusi na Uturuki, Putin alisema Moscow "inaridhika" na uhusiano na Ankara.

"Yote haya yanatokea kutokana na uongozi na kuungwa mkono na rafiki yetu, Rais wa Jamhuri ya Uturuki," alisema.

Akibainisha kushuka kidogo kwa biashara baina ya nchi hizo mwanzoni mwa mwaka huu, Putin alisema Moscow inahusisha hili hasa na marekebisho ya bei za bidhaa kuu zinazouzwa na kuagizwa na Urusi.

"Ni matumaini yangu kuwa tutaweza kurekebisha hali hii katika siku za usoni na kila kitu kitakuwa sawa kama mwaka jana," alisema.

Akizungumzia mkutano wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai (SCO) huko Astana, mji mkuu wa Kazakhstan, mapema mwezi ujao, Putin alisema: "Ninatumai kwamba katika siku za usoni ... Julai 3-4 (Erdogan) atakuwa Astana, na kama ninavyojua, kama sehemu ya tukio la kimataifa, na tutapata fursa ya kukutana naye na kujadili masuala yote ya sasa.”

TRT Afrika