Viongozi wa dunia wametuma pongezi zao kwa rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan kufuatia ushindi wake katika duru ya pili ya uchaguzi wa urais.
Erdogan alipata ushindi mkubwa siku ya Jumapili, kwa kujikusanyia zaidi ya kura milioni 27 mbele ya mgombea wa upinzani Kemal Kilicdaroglu akiwa na zaidi ya kura milioni 25.
Wakati viongozi wa kimataifa wakijumuika katika kupeleka pongezi zao kwa Erdogan, Emir wa Qatar Tamim bin Hamad alikuwa kiongozi wa kwanza wa dunia kumpongeza Erdogan, akiandika kwenye mitandao ya kijamii.
"Ndugu yangu mpendwa Recep Tayyip Erdogan, hongera kwa ushindi wako - nakutakia mafanikio katika muhula wako mpya - natamani uhusiano wetu mzuri uendelee kuboresha maendeleo na ukuaji wa nchi zetu."
Chini ya uongozi wa Erdogan, Uturuki ilikuwa moja ya nchi za kwanza zilizoisaidia Qatar baada ya kizuizi kilichowekwa na majirani zake wa Ghuba mnamo 2017.
Waziri Mkuu wa Palestina Mohammad Shtayyeh pia alitoa pongezi kwa Erdogan na watu wa Uturuki kwa ushindi wa urais katika uchaguzi huo.
Wakati huo huo, Rais wa Urusi Vladimir Putin alisema ushindi wa uchaguzi "ni matokeo ya asili ya kazi yako ya kujitolea" ya Erdogan kama kiongozi wa Uturuki.
"Tunathamini sana mchango wako wa kibinafsi katika kuimarisha uhusiano wa kirafiki kati ya Urusi na Uturuki na ushirikiano wa kunufaishana katika maeneo mbalimbali," Putin alisema.
Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orban pia alituma ujumbe wake, akisifu, "ushindi wa uchaguzi usio na shaka" wa Erdogan.
Katika ujumbe mrefu uliotumwa kwenye Twitter, Waziri Mkuu wa Pakistani Shehbaz Sharif aliutaja ushindi wa Erdogan kuwa "wa kihistoria".
"Yeye ni mmoja wa viongozi wachache wa dunia ambao siasa zao zimejikita katika utumishi wa umma. Amekuwa nguzo ya nguvu kwa Waislamu wanaokandamizwa na sauti ya dhati kwa haki zao zisizoweza kuondolewa."
"Ninatazamia kwa hamu kufanya kazi naye ili kuimarisha zaidi ushirikiano wetu wa kimkakati sambamba na udugu bora kati ya watu wetu wawili."
Wakati huo huo, rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud pia amempongeza rais Erdogan.
Video zilizochapishwa kwenye mitandao ya kijamii pia zilionyesha sherehe nchini Syria na Azerbaijan baada ya ushindi wa Erdogan kuwekwa wazi.
Rais wa Azerbaijan Ilham Aliyev pia alimpongeza Rais Erdogan kwa kuchaguliwa tena kwa njia ya simu, akimkaribisha kutembelea Baku katika siku za usoni.