Rais wa Uturuki Tayyip Erdogan akutana na waziri wa mambo ya nje wa China Wang Yi mjini Ankara / Picha: Reuters

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan alipokea Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi katika mji mkuu Ankara kwa mazungumzo.

Mapema siku ya Jumatano, Wang, ambaye pia ni mwanachama wa kamati ya kisiasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC), alikutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Hakan Fidan kujadili uhusiano wa pande mbili, masuala ya kikanda na kimataifa.

"Katika mkutano huo, ambapo pande zote za uhusiano kati ya Uturuki na China zilijadiliwa, njia za kutumia vyombo vya mazungumzo na mashauriano kati ya nchi hizo mbili kwa njia iliyo na ufanisi zaidi zilijadiliwa, kama vile Kamati ya Ushirikiano wa Serikali kwa Serikali, Mfumo wa Mashauriano kati ya Mawaziri wa Mambo ya Nje, Mashauriano ya Konsuli, Tume ya Pamoja ya Uchumi," ilieleza taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Uturuki baada ya mkutano.

Kuhusu juhudi za kuafikiana na Mpango wa Barabara na Ukanda wa China na Mpango wa Korido ya Kati ya Uturuki, Erdogan alisema wanataka kufanya mkutano wa kwanza wa kikundi cha kazi cha ngazi ya juu kilichoundwa kwa kusudi hili, iliongeza taarifa hiyo.

Erdogan alisema alituma ujumbe wake wa kutaka ushirikiano imara zaidi kati ya nchi hizo mbili, ambazo zina ushawishi mkubwa katika maswala ya kimataifa na kikanda, ilisema Kurugenzi hiyo.

Njia za kufikia muundo wa biashara wa pande mbili ulio na usawa na endelevu kati ya Uturuki na China na masuala ya kuongeza uwekezaji kwa pande zote yalijadiliwa pia.

Jumanne, China ilimwondoa Waziri wa Mambo ya Nje Qin Gang, ambaye hakuonekana kwa umma kwa mwezi mmoja, na kumteua tena Wang katika nafasi yake ya zamani kama mkuu wa kidiplomasia wa nchi hiyo.

Mahusiano ya kidiplomasia kati ya Uturuki na China yalianzishwa mwaka 1971. Mwaka 2010, uhusiano uliongezwa hadi kiwango cha ushirikiano mkakati.

TRT Afrika