Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu, “anayepeleka ukanda wetu na dunia nzima katika janga kubwa, lazima adhibitiwe na akomeshwe,” Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amesema.
"Mtu huyu aitwaye Netanyahu, mwovu na mwenye kiu ya kumwaga damu anapeleka ukanda wetu na dunia nzima kwa ujumla katika janga kubwa, lazima adhibitiwe,” alisema Erdogan katika risala yake aliyoitia kwenye mji mkuu wa Ankara.
"Uturuki inapinga ukandamizaji, mauaji na dhuluma ambayo imekuwa ikiendelea kwa miaka 76, na inasimama pamoja na watu wa Palestina," aliongeza .
Kuhusu mapambano dhidi ya ugaidi, Erdogan alisema: "Uturuki haiwezi kupata amani au kujisikia salama hadi vyanzo vinavyozalisha ugaidi kaskazini mwa Iraq na Syria vitakapoisha."
Zaidi ya Wapalestina 36,400 wameuawa huko Gaza katika hujuma mbaya ya Israeli huko Gaza tangu Oktoba 7 iliyopita kufuatia shambulio la Hamas. Wengi wa waliouawa ni wanawake na watoto, huku wengine zaidi ya 82,600 wakijeruhiwa, kulingana na mamlaka ya afya ya eneo hilo.
Maeneo makubwa ya Gaza yamegeuka kuwa magofu huku kukiwa na vizuizi kutoka Israeli vya upatikanaji wa chakula, maji safi, na dawa.
Israeli inashutumiwa kwa mauaji ya halaiki katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ), ambayo uamuzi wake wa hivi karibuni iliiamuru Tel Aviv kusitisha mara moja operesheni yake huko Rafah, ambapo zaidi ya Wapalestina milioni 1 walikuwa wametafuta hifadhi kutokana na vita vya mauaji ya halaiki vinavyoendelea.