Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ameilaumu Israeli kwa kutumia migogoro ya kikanda kama kisingizio cha kuendeleza "ukaaji wa kibabe."
“Yemen, Syria, na Iran ni visingizio tu,” alisema Erdogan siku ya Jumamosi. “Serikali ya Israeli kila siku inakuja na visingizio vipya vya kuhalalisha na kuendeleza uvamizi wake,” aliongeza Rais Erdogan wakati akizungumza katika mkutano wa chama cha AK jijini Istanbul.
Erdogan alisema kuwa mataifa ya magharibi yanaendelea kudharau yanayofanywa na Israeli kutokana na hatia ya maangamizi makuu dhidi ya Wayahudi. Pia amewataka washirika wa Israeli kuchukua hatua za haraka kudhibiti vitendo vya Israeli.
Erdogan pia alisisitizia mapambano ya Wapalestina dhidi ya vitendo vya Israeli, toka Oktoba 7.
“Ndugu zetu wa Gaza wamekuwa wakipambana na mavamizi wa Kisayni kwa siku 364 sasa,” alisema.
Rais Erdogan pia amesisitiza kuwa Ankara itaendelea kuiunga mkono Gaza kwa njia yoyote ile
“Tunasimama imara mahali pale pale leo tuliposimama siku ya kwanza. Tunatetea maadili yale yale leo tuliyotetea siku ya kwanza,” alisema.
Uturuki huwa hachelei kusema mambo yale yale kwenye jukwaa la Umoja wa Mataifa kama inavyouambia umma wa ndani, aliongeza Erdogan.
Kulingana na Erdogan, Uturuki ni nchi pekee iliyoiwekea Israeli vikwazo vya kiuchumi.