Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ameikosoa Israeli kufuatia mauaji ya 'kinyama' ya Aysenur Ezgi Eygi, mwanaharakati wa Kituruki na Kimarekani, ambaye aliuwawa na majeshi ya Israeli siku ya Ijumaa, wakati wa maandamano katika eneo linalokaliwa la West Bank.
Akizungumza siku ya Jumamosi jijini Istanbul, Erdogan alisema kuwa, kwa sasa Israeli ina nia ya kufanya mauaji ya kimbari katika maeneo ya West Bank na Gaza, ikiwa ni pamoja na kutwaa maeneo hayo mawili.
"Jana, (Israeli) walimuua mtoto wetu mdogo, Aysenur Ezgi Eygi. Hadi sasa, wameua zaidi ya raia 40,000 wasio na hatia, wakiwemo watoto 17,000,” Erdogan alisema. "Wanashambulia kinyama na kumwaga damu ovyo, iwe ni watoto, wanawake, vijana au wazee."
Eygi alipigwa risasi na kuuwawa na majeshi ya Israeli siku ya Ijumaa wakati akishiriki katika maandamano ya kupinga utanuzi wa makazi katika mji wa Beita, ulio karibu na Nablus kaskazini mwa West Bank.
Ripoti ya madaktari ilithibitisha kuwa Eygi aliuwawa na risasi aliyopigwa kichwani, gavana wa Ghassan Daghlas alisema siku ya Jumamosi.
Jukumu la kusimama dhidi ya ugaidi wa Kiisraeli ni la Kiislamu na la kitaifa, alisema rais huyo.
Erdogan pia alisisitiza mpango wa kidiplomasia wa Uturuki na Misri ambao unalenga kuwanufaisha watu wa Gaza na Palestina.