Polisi wa Uturuki wamemkamata mshukiwa wa kigaidi wa Daesh mjini Istanbul.
Shamil Hukumatov wa Tajikistan ni gaidi "mwenye cheo cha juu" wa Daesh-K na anaaminika kuhusika na usajili wa wanajeshi wapya wa kundi hilo la kigaidi na pia kuwapa pesa, duru za usalama zililiambia Shirika la Anadolu siku ya Alhamisi.
Vyanzo vya habari vinasema kuwa serikali ya Tajikistan imetoa hati ya kukamatwa kwa Hukumatov, ambaye pia anajulikana kwa jina lake la "Abu Miskin," kwa madai ya shughuli za uasi nchini humo.
Daesh waliunda kundi la kigaidi la Daesh-K, ambalo pia linajulikana kama IS-K, mnamo Juni 2014, ambalo linajumuisha Afghanistan, Pakistan, na nchi zingine jirani za Kusini na Kati mwa Asia.
Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari, mkuu wa kundi la kigaidi la Daesh-K Sanaullah Ghaffari, ambaye pia anajulikana kama Shahab Al Muhajir, aliuawa katika mkoa wa Kunar kaskazini magharibi mwa Afghanistan katika wiki ya kwanza ya mwezi Juni.
Alihusika na mashambulizi kadhaa mabaya nchini Afghanistan, ikiwa ni pamoja na shambulio la bomu la kujitoa mhanga katika Uwanja wa Ndege wa Kabul mnamo Agosti 2021 na kuwaua zaidi ya watu 180. Utawala wa muda wa Taliban, hata hivyo, bado haujathibitisha kifo chake.
Wakati wa uvamizi wa Alhamisi, polisi wa Istanbul walimzuilia mke wa Hukumatov, aliyetambuliwa tu na herufi za kwanza kama M.S., na kupata idadi kubwa ya habari, hati na nyenzo zinazohusiana na kundi hilo la kigaidi wakati wa upekuzi katika makazi yao, kulingana na vyanzo hivi.
Hukumatov alirudishwa rumande na mahakama ya eneo hilo baada ya kukamilisha taratibu zinazohitajika katika kituo cha polisi, huku mkewe, M.S., akiachiliwa chini ya uangalizi wa mahakama, waliongeza.
Mnamo 2013, Uturuki ilikua miongoni mwa nchi za kwanza kutangaza Daesh kuwa shirika la kigaidi.
Tangu wakati huo nchi hiyo imeshambuliwa na kundi hilo la kigaidi mara kadhaa, huku zaidi ya watu 300 wakiuawa na mamia zaidi kujeruhiwa katika mashambulizi 10 ya kujitoa mhanga, mashambulizi saba ya mabomu na mashambulizi manne ya silaha.
Kujibu, Türkiye ilianzisha operesheni za kupambana na ugaidi ndani na nje ya nchi ili kuzuia mashambulizi zaidi.