Kikao kati ya Fidan na Haniya kinakuja baada ya shambulio baya la Israeli katika kambi ya wakimbizi ya Nuseirat katikati ya Gaza /Picha: AA  

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Hakan Fidan amefanya kikao nchini Qatar na kiongozi wa kikundi cha Palestina cha Hamas, kulingana na Wizara hiyo.

Kikao hiki kimefanyika mjini Doha baada ya Fidan kushiriki katika mkutano wa sita wa mawaziri wa mambo ya nje kati ya nchi za Baraza la Ushirikiano la Uturuki na Ghuba(GCC) kwa majadiliano ya ngazi ya juu ya kimkakati.

"Waziri wa Mambo ya Nje Hakan Fidan amekutana na Ismail Haniya, kiongozi wa Hamas, wakati wa mkutano wa sita wa mawaziri wa mambo ya nje kati ya nchi za Baraza la Ushirikiano la Uturuki na Ghuba(GCC) mjini Doha," ilisema taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje siku ya Jumapili kwenye ukurasa wake wa X baada ya mkutano huo .

Mkutano kati ya Fidan na Haniya unafanyika baada ya mashambulizi ya kikatili ya Israel dhidi ya kambi ya wakimbizi ya Nuseirat katikati mwa Gaza, na kusababisha vifo vya makumi ya Wapalestina na kujeruhi wengine wengi.

Idadi ya waliofariki kutokana na shambulizi la Israeli kwenye kambi ya wakimbizi ya Nuseirat katikati mwa Gaza imeongezeka hadi kufikia 274, huku wengine karibu 700 wakijeruhiwa, kwa mujibu wa wizara ya afya ya serikali ya Palestina.

Mapema Jumapili, Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki ililaani shambulio hilo kati kambi ya wakimbizi ya Nuseirat iliyoko Gaza.

"Israeli imeongeza orodha ya uhalifu wa kivita inaoendelea kuufanya huko Gaza kufuatia shambulio la hivi karibuni ," wizara hiyo ilisema.

Serikali ya Uturuki imetoa wito kwa taasisi za kimataifa, hususani Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuchukua hatua stahiki kusitisha mashambulizi ya Israeli.

"Tunazitaka taasisi zenye wajibu wa kulinda amani na usalama wa dunia, hususani Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kutimiza wajibu wao na kusitisha uhalifu wa Israeli," ilisomeka taarifa hiyo.

TRT Afrika