Mke wa Rais Emine Erdogan ameongoza mkutano wa tatu wa Baraza la Ushauri la Umoja wa Mataifa la Watu Mashuhuri la kushughulikia usafi wa mazingira duniani, katika ofisi ya Rais ya Dolmabahce jijini Istanbul.
Katika mkutano huo, Mke wa Rais alisisitiza umoja wa kidunia katika kupambana na mabadiliko ya tabia nchi na usafi wa mazingira, wakati akitoa risala yake siku ya Ijumaa.
Erdogan aligusia changamoto mbalimbali zinazosababishwa janga la uchafuzi wa mazingira, akitaka hatua za haraka na za pamoja kuchukuliwa.
"Kupata dunia yenye usawa bado inawezekana, licha ya yote haya," alisema.
"Jambo hili litafanikiwa kupitia kwa jitihada zetu. Sote ni washirika katika lengo hili."
Sababu za kihistoria na za sasa
Erdogan aligusia ukubwa wa tatizo la mazingira linalotokana na matatizo ya ki kihistoria na ya kisasa.
Akirejea athari za vita ya pili ya dunia, alisema kuwa baadhi ya athari za kimazingira bado hazijatatuliwa.
Akiangazia migogoro ya siku za karibuni, alisema , “Siku hizi, nchi moja inaweza kurusha mabomu yenye ukubwa sawa na matatu ya Atomiki katika eneo la raia, nusu ya ukubwa wa eneo la New York," akizungumzia mashambulizi ya Israeli katika eneo la Gaza.
"Mpango wa Mazingira wa Umoja wa Mataifa unasema kuwa inaweza kuchukua miongo kadhaa kusafisha uchafu uliotokana na vita vya Gaza. Hapa tunazungumzia karibu tani milioni 39 za uchafu, huku urejelezaji wake ukichukua miaka kama 45,” alisema Mke wa Rais wa Uturuki.
Alisisitiza kuwa ni lazima rasilimali zitumike ile kuiponya dunia, na sio kuizidishia mateso, akisisitizia haja ya hatua za kidunia kulinda vizazi vijavyo.
Mabadiliko ya tabia nchi
Erdogan aligusia athari za kutisha za majanga yatokanayo na mabadiliko ya tabia nchi, akisema kuwa yamewafanya watu zaidi ya milioni 120 kukosa makazi ndani ya mwaka huu peke yake.
“Ndani ya miaka mitano ijayo, tutafikia malengo endelevu ya maendeleo, hata hivyo bado tuko mbali kutimiza ahadi tulizojiwekea,” alisema.
Pia aliangazia matumizi yaliyozidi ya rasilimali ulimwenguni, hususani siku ambayo mahitaji ya dunia yalizidi uwezo.
“Toka kipindi hicho, tumeendelea kufanya wizi wa rasilimali za baadaye,” alionya.
Usafi wa mazingira
Mke wa Rais wa Uturuki Erdogan alielezea usimamizi wa mazingira kama falsafa ya kimageuzi ambayo sio tu itapunguza makali ya majanga ya kimazingira, bali pia itabadilisha namna ya matumizi.
“Usimamizi wa mazingira hutoa taswira kamili ya kubadilisha hali nzima ya uharibifu na kutoa nafasi kwa uendelevu wa uhai,” alisema.
Aliitaka Bodi hiyo ya Ushauri kuendeleza ukuzaji wa falsafa hiyo ulimwenguni, akisisitiza umuhimu wa Machi 30, kama fursa ya kuongeza uelewa na kusukuma mbele mapambano hayo.
Wakati akihitimisha risala yake, Erdogan ametaka kuwepo kwa uongozi dhabiti wa kusimamia utekelezaji huo kutoka kanda tofauti na kuleta matokeo tofauti yenye muelekeo mmoja.
Hali kadhalika, aliweka wazi mpango wa mkutano ujao wa Usafi wa Mazingira kwa mwaka 2025, ambao utazileta pamoja nchi, sekta na mashirika tofauti kusukuma mbele ajenda hiyo.
“Licha ya majanga yanayotukabili, bado tunaendelea kushikilia matumaini yetu,” alihitimisha. “Penye nia, pana njia.”