Mahakama kuu ya Bern Canton nchini Uswizi ilibatilisha kuachiwa huru kwa washtakiwa wanne waliohusika na kuonesha bango lililomlenga Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan wakati wa mkutano wa hadhara miaka saba iliyopita, ripoti za vyombo vya habari zimesema.
Uamuzi huo wa Alhamisi ni kubatilishwa kwa hukumu ya mwaka wa 2022, ambapo washtakiwa waliachiliwa huru, kulingana na ripoti kutoka gazeti la Tages-Anzeiger na Swissinfo.ch.
Kila mshtakiwa ametozwa faini ya viwango tofauti, vya jumla ya Faranga 11,000 za Uswisi (dola 12,246), kwa kuhusika kwao katika kubeba bango hilo lenye ujumbe wenye utata.
Hukumu hiyo ilitokana na tathmini ya bango hilo, lililoonesha bunduki iliyoelekezwa kwenye kichwa cha Rais Erdogan, ikiambatana na neno "kuua."
Mahakama ilielezea ugumu wa kutafsiri neno "kuua" katika muktadha mwingine wowote isipokuwa kama uchochezi wa moja kwa moja wa ghasia dhidi ya rais wa Uturuki.
"Taarifa hiyo haiwezi kuchukuliwa kuwa haina upendeleo na inaweza kutafsiriwa kama wito wa mauaji," ulisema uamuzi huo pasipo na shaka yoyote.
'Uchochezi wa mauaji'
Vilevile, mahakama hiyo ilisisitiza kwamba uchochezi huo wa kufanya mauaji hauwezi kukingwa chini ya kivuli cha uhuru wa kujieleza au kukusanyika.
Kesi hiyo inatokana na maandamano ambapo makundi ya mrengo wa kushoto nchini Uswisi, pamoja na wafuasi wa makundi ya kigaidi ya PKK, DHKP-C, na YPG, yalikusanyika Machi 25, 2017.
Kati ya mabango na bendera zilizobebwa wakati wa maandamano hayo lilikuwa na picha ya Erdogan huku bunduki ikiwa imeelekezewa kichwani kwake na maneno yanayosomeka "Muue Erdogan" na "silaha zao wenyewe."