Kuondoka kwa Seneta wa Marekani anayepinga Uturuki ni manufaa kwa mahusiano na Marekani: Erdogan

Kuondoka kwa Seneta wa Marekani anayepinga Uturuki ni manufaa kwa mahusiano na Marekani: Erdogan

Rais wa Uturuki amesema kuwa kuondoka kwa muda kwa Seneta Menendez kutokana na tuhuma za ufisadi kutaharakisha mchakato wa kupata F-16s.
Rais Erdogan anasema Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu huenda akazuru Türkiye mwezi Oktoba au Novemba. / Picha: AA

Moja wapo ya changamoto zetu kuu kuhusu mapendekezo ya Uturuki ya kununua ndege za kivita za F-16 na vifaa vya kuboresha kutoka Marekani kwa matumizi yake binafsi imekuwa shughuli za Seneta wa Marekani Bob Menendez, alisema Rais Recep Tayyip Erdogan siku ya Jumanne, wakati wa kurejea kutoka kwa safari yake, mjini Nakhchivan huko Azerbaijan.

Akizungumza na vyombo vya habari wakati akirejea, Rais Erdogan alikuwa amesema kuwa likizo ya muda ya Seneta Menendez kutokana na madai ya ufisadi ingeharakisha mchakato wa Ututruki kupata F-16.

Wiki iliyopita, Seneta wa Marekani Bob Menendez na mkewe walifunguliwa mashtaka ya rushwa, kufuatia uchunguzi wa shirikisho kuhusu uhusiano wao na wafanyabiashara watatu wa New Jersey. Bob Menendez anajulikana kwa upinzani wake dhidi ya Uturuki na ukaribu wake na vuguvugu ya Cyprus ya Ugiriki na Armenia.

"Hata hivyo, suala la F-16 halitegemei Menendez pekee. Inajumuisha maeneo mbalimbali ambayo Waziri wetu wa Mambo ya Nje, Hakan Fidan, atasimamia. Sasa tunasubiri majibu ya wazi kutoka kwa Marekani kuhusu suala hili. Tunatumai kupata matokeo chanya bila kuchelewa sana,” Rais pia alisema.

"Mgogoro huu unasisitiza umuhimu wa kujitegemea katika sekta ya ulinzi kwa nchi yetu."

Marekani inaunganisha mauzo ya F-16 na ombi la Uswidi kujiunga na NATO.

Rais wa Uturuki aliendelea kusema kuwa Marekani imekuwa ikijaribu kuhusisha uuzaji wa ndege za kivita za F-16 na ombi la NATO la Sweden.

Sweden na Finland zilituma maombi ya kuwa mwanachama wa NATO mara tu baada ya Urusi kuanzisha vita vyake dhidi ya Ukraine mnamo Februari 2022.

Ingawa Uturuki imeidhinisha uanachama wa Finland katika NATO, inasubiri Uswidi kutii mkataba wa Juni 2022 wa pande tatu kushughulikia masuala ya usalama ya Ankara.

Ankara inaikosoa Sweden kwani kwa miongo kadhaa, nchi hiyo imekuwa ikihifadhi wanachama wa makundi mbalimbali ya kigaidi, ikiwa ni pamoja na miaka ya hivi karibuni PKK, pamoja na Shirika la Kigaidi la Fetullah (FETO), kundi lililoendesha jaribio la mapinduzi lililotibuka la 2016 huko nchini Uturuki.

Wakati Ankara imekuwa ikihusisha kuingia kwa Stockholm katika NATO na sharti la kukabiliana na makundi hayo ya kigaidi katika ardhi ya Sweden, Marekani imekuwa ikijaribu kuhusisha hatua ya Uturuki kuruhusu uanachama wa NATO na mauzo ya ndege zake za F-16, jambo alilolosukuma zaidi Seneta Menendez.

Baada ya mazungumzo ya zaidi ya mwaka mmoja, Erdogan alikubali kuiruhusu Sweden kuingia NATO mwezi Julai, na kukabidhi uamuzi wa mwisho kwa Bunge la Uturuki ili kuidhinishwa.

"Uamuzi kuhusu uanachama wa NATO wa Sweden utatolewa na Bunge Kuu la Uturuki. Bunge letu linafuatilia kwa karibu kila maendeleo yanayohusiana na suala hili,” Rais alisema wakati huo.

"Hatuwezi kurudisha Bunge letu nyuma," aliongeza.

Uhusiano na Israel

Katika hotuba iliyoangazia mada kadhaa, rais Erdogan pia alizungumzia uhusiano wa Uturuki na Israel. Alisema kuwa Uturuki na Israel zinashirikiana katika maeneo mengi, na kuna fursa za ushirikiano zaidi katika maeneo mapya pia.

"Hasa, kuna utafutaji wa vyanzo vya nishati, vilivyoathiriwa na mazingira ya vita vya baada ya Urusi-Ukraine, na Israel inatazamia kusafirisha rasilimali zake hadi Ulaya," alisema.

"Pia kuna fursa za ushirikiano katika shughuli za uchimbaji visima [katika Mediterania]. Tumewaagiza wenzetu husika kufanya tafiti za kiufundi kuhusu suala hili,” Rais alisema.

"Katika mikutano ijayo kati ya Uturuki na Israel, tutafafanua maelezo ya masuala kama vile njia, ratiba na maeneo ya kuchimba visima haraka iwezekanavyo."

Rais Erdogan pia alisema Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu huenda akazuru Uturuki mwezi Oktoba au Novemba.

Kufungua ukanda wa Zangezur na Azerbaijan

Rais pia alipongeza uhusiano na ushirikiano wa Uturuki na Azerbaijan, na akasema kwamba kuanzisha uhusiano wa moja kwa moja na Nakhchivan na mikoa mengine ya Azerbaijan kupitia mitandao ya barabara na reli kutaimarisha uhusiano huo.

Ukanda wa Zangezur uliopangwa - barabara isiyozuiliwa kupitia eneo la Armenia, inayounganisha Azerbaijan na eneo lake la Nakhchivan - pia itaunganisha Azerbaijan moja kwa moja na Uturuki Mashariki.

Eneo la Zangezur awali lilikuwa sehemu ya Azerbaijan, ingawa Wasovieti waliipa Armenia katika miaka ya 1920, na kuinyima Azerbaijan njia ya moja kwa moja ya nchi kavu kuelekea Nakhchivan.

Kufuatia vita vyake vya siku 44 na Armenia katika msimu wa vuli wa 2020, Azerbaijan imezingatia viunganisho vilivyopangwa, pamoja na barabara na reli ya kilomita 43 kupitia ukanda.

"Kwa uhusiano huu mkubwa, tunalenga kupata maendeleo mengi zaidi katika maeneo mbalimbali katika siku zijazo kuliko tulivyofanya kwa kutembea, ikiwezekana hata kukimbia. Kwa hivyo, tutafanya kila juhudi kuharakisha ufunguzi wa ukanda huu,” alisema Erdogan.

"Utekelezaji wa ukanda huu ni wa umuhimu wa kimkakati kwa Uturuki na Azerbaijan, na lazima ukamilike. Ukanda huu unapofanya kazi, gari au treni inayotoka Baku itaweza kufika Kars (kaskazini mashariki mwa Uturuki) moja kwa moja," alisema.

"Uhusiano kati ya Uturuki na Azabajani utakua na nguvu zaidi."

Suala la Cyprus

Rais Erdogan alisema kuwa kuitambua Jamhuri ya Uturuki ya Cyprus ya Kaskazini (TRNC) ndilo chaguo linalofaa zaidi kwa mataifa yote yanayotafuta amani na utulivu wa kudumu katika kisiwa cha Cyprus.

Uturuki imekuwa ikizikosoa nchi za Magharibi kwa mtazamo wake wa kuegemea upande wa mzozo katika kisiwa cha Cyprus, ambacho kimegawanyika mara mbili, huku Waturuki wa Cyprus wakiwa upande wa kaskazini na Cyprus za Ugiriki upande wa kusini.

"Pamoja na TRNC, tumegundua njia zote za suluhisho. Tumezingatia kanuni zote, pamoja na ile ya kuunda shirikisho, kwa dhati," Erdogan alisema.

"Lakini sasa, imekuwa wazi na dhahiri kwamba hakuna chaguo isipokuwa suluhisho la serikali mbili nchini Cyprus. Hakuna anayepaswa kutarajia sisi kupuuza haki za TRNC au kuwatelekeza.”

TRT World