Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amekuwa mwenyeji wa Katibu Mkuu wa NATO Mark Rutte jijini Ankara.
Kikao chao cha jumatatu kiliangazia mambo mbalimbali kama vile vita vya Ukraine na migogoro ya Mashariki ya Kati.
Kabla ya kikao hicho, Rutte alisema: “Nategemea kukutana na Rais Erdogan kujadiliana changamoto za kiusalama, ikiwemo ugaidi, vita vya Ukraine na mgogoro wa Mashariki ya Kati.”
“Katika dunia hii isiyotabirika, Uturuki inachangia pakubwa katika umoja wetu,” alisema.
Rutte alisema kuwa Uturuki ina jeshi la pili kwa ukubwa ndani ya NATO, ikiwa ni mwanachama kwa muda wa miaka 70.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Hakan Fidan na Waziri wa Ulinzi, Yasar Guler walihudhuria kikao hicho kilichofanyika katika jumba la Rais. Hii ni mara ya kwanza kwa Rutte kuitembelea Uturuki katika nafasi yake kama Katibu Mkuu wa NATO, taarifa ya ofisi ya Rais wa Uturuki ilisema.
Kwa namna ya pekee, Fidan alipata fursa ya kufanya mazungumzo na kiongozi huyo wa NATO, Wizara ya Mambo ya Nje ilisema.
Hata hivyo, ajenda za mikutano hiyo hazikuwekwa wazi.
Rutte, ambaye ni Waziri Mkuu wa zamani wa Uholanzi, anakuwa Katibu Mkuu wa 14 wa NATO, akichukua nafasi ya Jens Stoltenberg.
Uturuki imekuwa mwanachama wa NATO kwa kipindi cha zaidi ya miaka 70.