Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amelaani mashambulio yasiyokoma ya Israel dhidi ya Wapalestina katika eneo lililozingirwa la Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, akitaja vitendo hivi kuwa doa lisilofutika katika historia ya binadamu.
Israel imekuwa ikitekeleza mauaji haya kwa kuungwa mkono na nchi za Magharibi, Erdogan aliambia kundi la Chama cha Haki na Maendeleo (AK) kilichokutana katika Bunge la Uturuki siku ya Jumatano.
Akisisitiza kwamba wanajeshi wa Israel wameua zaidi ya watoto 14,000 wasio na hatia huko Gaza tangu Oktoba 7, Erdogan alishangazwa na ukatali wa Tel Aviv, akisema umeshinda ule wa Ujerumani ya Nazi kama ulivyoongozwa na Adolf Hitler.
Akisema kwamba hakuna anayeweza kuhoji unyeti wa Uturuki katika suala la Palestina, Erdogan aliongeza kuwa kadhia ya Palestina iliyapa maisha yake maana mpya.
"Maadamu Mwenyezi Mungu atanijalia uhai, nitaendelea kutetea mapambano ya Palestina, na nitakuwa sauti ya watu wanaodhulumiwa wa Palestina," aliongeza.
Rais alikumbuka miaka 15 iliyopita, katika Kongamano la Kiuchumi la Dunia la 2009 huko Davos, Uswizi, wakati alipinga uongozi wa Israeli na ukandamizaji wake kwa Wapalestina, kwa kupinga, "Dakika moja!"
"Wakati wengine hawakuzungumza , tulisimama na kusema: 'Hamas si shirika la kigaidi, bali ni kundi la upinzani.' Tuliwasilisha ramani katika Umoja wa Mataifa zinazoonyesha jinsi Israel ilivyozikalia ardhi ya Palestina hatua kwa hatua katika kipindi cha miaka 70," aliongeza.
"Tulikuwa pamoja na ndugu zetu wapalestiina katika kila hali, hususani katika mapito yao magumu. Tumejipanga kuendelea kuwasaidia watu wa Gaza wanaonewa," alisisitiza Erdogan.
Alisisitiza azma ya Uturuki ya kutetea kwa ujasiri mapambano ya uhuru wa Palestina kwa hali yoyote.
Haniya kuzuru Uturuki
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Hakan Fidan na Ismail Haniya, kiongozi wa tawi la Hamas walikutana jijini Doha siku ya Jumatano kujadili yanayoendelea Gaza, kulingana na vyanzo vya kidiplomasia.
Fidan alifanya mkutano na Haniya na ujumbe wake, na kujadiliana juu ya masuala yanayohusu msaada wa kibinadamu kwa Gaza, kusitisha mapigano, pamoja na mateka, vyanzo viliongeza.
Kulingana na taarifa kutoka kwa Erdogan, Haniya anatazamiwa kuzuru Uturuki wikendi hii.
Kulingana na Umoja wa Mataiafa, vita vya Israel dhidi ya Gaza vimesababisha asilimia 85 ya wakazi wa eneo hilo kuwa wakimbizi wa ndani huku kukiwa na uhaba mkubwa wa chakula, maji safi na dawa, huku zaidi ya asilimia 60 ya miundombinu ya eneo hilo ikiharibiwa.
Israel inashutumiwa mauaji ya halaiki katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki. Uamuzi wa Januari uliitaka Tel Aviv kusitisha vitendo vya mauaji ya halaiki na kuchukua hatua ya kuhakikisha kuwa misaada inatolewa kwa raia wa Gaza.