Altun alionesha matumaini yake ya mabadiliko ya kifikra ndani ya vijana wa Marekani kuhusu mgogoro kati ya Israeli na Palestina./ Picha: AA  

Mkuu wa Mawasilino wa Uturuki, Fahrettin Altun, ameelezea kauli ya hivi karibuni ya Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu aliyoitoa ndani ya bunge la Marekani, kama doa kwa muhimili huo unaojinasibu kuimarisha haki za kibinadamu na tunu za demokrasia.

"Hotuba ya Waziri Mkuu wa Israeli kwa Bunge la Marekani ni doa kubwa kwa chombo hiki kinachodai kutetea haki za binadamu na kuzingatia maadili ya kidemokrasia. Kwa kuwa mwenyeji wa mwanasiasa anayehusika na uhalifu wa kivita, Washington inatuma ujumbe kwa ulimwengu kwamba haijali chochote kuhusu maisha ya raia wasio na hatia," Altun alisema kwenye ukurasa wa X siku ya Alhamisi.

Altun amelilaani Bunge la Marekani kwa kumpa Netanyahu jukwaa la kueneza kile alichokitaja kama propaganda, huku akiwadharau waandamanaji wa amani wa Marekani. "Kujihusisha kwa baadhi ya wanasiasa wa Marekani katika uhalifu wa serikali ya Israeli kwa manufaa ya kisiasa kutakuwa na madhara kwa uaminifu wa Marekani duniani kote."

'Bunge la Congress limeeneza vita hivi'

Licha ya uungwaji mkono mkubwa alioupata Netanyahu, Altun alikiri baadhi ya wanasiasa wa Marekani ambao ama walipinga au kupinga hotuba ya waziri mkuu wa Israeli.

Alisifia uamuzi wa viongozi hao, akisisitiza kuwa hotuba hiyo "ilijaa uongo" na "chuki dhidi ya Wapalestina," na kumkosoa Netanyahu kwa kutumia maneno yenye kuwakandamiza Wapalestina.

"Vikosi vya usalama vya Israeli chini ya serikali ya Netanyahu vimekuwa vikifanya uhalifu usioelezeka huko Palestina. Bunge la Marekani limewezesha uwepo wa vita hivyo kwa kutoa msaada wa kifedha, silaha na risasi. Juhudi za kuweka masharti ya msaada huo kwa Israel kuhusu haki za binadamu zimeshindwa kabisa. lazima ikome ikiwa Marekani inalenga kudai aina yoyote ya uongozi wa kimaadili au uhalali katika nyanja ya kimataifa," Altun alitangaza.

'Jitahada za Uturuki za mataifa mawili'

Altun alionesha matumaini kuhusu mabadiliko ya mitazamo miongoni mwa vizazi vichanga nchini Marekani kuhusu mzozo wa Israeli na Palestina, akisisitiza ufahamu wao unaoongezeka kuhusu mauaji ya kimbari huko Palestina.

Amesisitiza kuwa hali ya sasa si endelevu na akatabiri kuwa Wapalestina watapata mamlaka yao kamili. Amewataka wanasiasa wa Marekani kutambua kwamba kuunga mkono serikali ya Netanyahu ni kinyume na maslahi na maadili ya Marekani.

Katika kuonesha mshikamano, Altun alithibitisha dhamira ya Uturuki katika utatuzi wa haki wa mzozo wa Israel na Palestina. "Kwa mara nyingine tena, tunatangaza mshikamano na wale wanaounga mkono utatuzi wa haki wa mzozo wa Israeli na Palestina. Tutafanya kazi kwa bidii kuufanya ukweli hata kama serikali ya Netanyahu, pamoja na washirika wake katika Congress ya Marekani, wanapinga."

Altun alihitimisha taarifa yake kwa kulaani matumizi ya shutuma za chuki dhidi ya Wayahudi kuwanyamazisha wakosoaji wa sera za Israeli na kusifu ufahamu wa jumuiya ya kimataifa kuhusu athari za mashambulizi ya Israeli kwa raia wasio na hatia.

Alisisitiza juhudi za Uturuki za kufikia suluhu ya mataifa mawili, na Palestina yenye mamlaka kamili inayoishi kwa amani pamoja na majirani zake.

"Dhamira ya dunia iko upande wa Palestina huru. Hakuna uhalali wa mauaji ya kikabila na mauaji ya kimbari," aliongeza.

TRT Afrika