Mnamo 2019, Erkan alijumuishwa katika orodha ya Crain ya "Wanawake Mashuhuri wa Benki na Fedha" na "Wanawake wa Kutazama" ya Benki ya Amerika. / Picha: AA

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amemchagua gwiji wa maswala ya kibenki mwenye uzoefu Hafize Gaye Erkan kumrithi Sahap Kavcioglu kama gavana wa Benki Kuu ya Uturuki, Gazeti Rasmi la nchi hiyo lilitangaza.

Erkan, 41, alipata shahada ya kwanza katika uhandisi wa viwanda kutoka Chuo Kikuu cha Bogazici cha Istanbul, akihitimu kama mwanafunzi bora, na alipata udaktari katika shughuli za utafiti na uhandisi wa kifedha katika Chuo Kikuu cha Princeton.

Erkan pia alikamilisha programu mbili za mafunzo ya juu ya sayansi ya usimamizi katika Shule ya Biashara ya Harvard na uongozi katika Chuo Kikuu cha Stanford.

Akiwa na idadi ya nyadhifa za juu katika makampuni makubwa chini ya jina lake, aliwahi kuwa Mkurugenzi Mtendaji mwenza wa First Republic Bank yenye makao yake Marekani na mjumbe wa bodi ya wakurugenzi huko Marsh McLennan, kampuni ya huduma katika nyanja za hatarishi, mikakati na bima, mkurugenzi mkuu wa benki ya uwekezaji Goldman Sachs, na mjumbe wa bodi ya kampuni ya vito ya Tiffany & Co.

Erkan, mwanamke wa kwanza chini ya umri wa miaka 40 kushikilia cheo cha rais au Mkurugenzi Mtendaji katika mojawapo ya benki 100 kubwa zaidi za Amerika, aliwekwa orodha ya "40 Under 40" ya San Francisco Business Times na Crain New York Business.

Mnamo 2019, Erkan alijumuishwa katika orodha ya Crain ya "Wanawake Mashuhuri wa Benki na Fedha" na "Wanawake wa Kutazama" ya Benki ya Marekani.

Erkan anajivunia utaalam katika benki, uwekezaji, udhibiti wa hatari, teknolojia, na uvumbuzi wa kidijitali, na pia anahudumu katika Baraza la Ushauri la Idara ya Utafiti wa Uendeshaji na Uhandisi wa Fedha ya Chuo Kikuu cha Princeton.

Baada ya Kavcioglu kutajwa kwenye usukani wa Benki Kuu mnamo Machi 2021, kamati ya sera ya fedha ya benki hiyo ilipunguza polepole kiwango cha riba yake kutoka asilimia 19 hadi asilimia 8.5.

Wiki iliyopita, Erdogan pia alitangaza kuwa Mehmet Simsek anamrithi Nureddin Nebati kama Waziri wa Hazina na Fedha.

Katika hafla ya makabidhiano, Simsek alisema: "Uturuki haina chaguo ila kurudi kwenye msingi mzuri.

“Sera yetu kuu itakuwa ni kuisaidia Benki Kuu yetu katika vita dhidi ya mfumuko wa bei kupitia sera ya fedha na mageuzi ya kimuundo yatakayo tekelezwa.

TRT World