Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Hakan Fidan amekutana na Meja Jenerali wa Misri Khaled Megawer, gavana wa Sinai Kaskazini, katika eneo la El Arish.
Kufuatia kukutana kwao, Fidan alisafiri hadi kwenye mpaka wa kivuko cha Rafah siku ya Alhamisi, ambacho kilikuwa kimefungwa kupitisha msaada wa kibinadamu ndani ya Gaza kutokea Misri kuanzia mwezi Mei.
Ziara ya Fidan ililenga kupata taarifa muhimu kuhusu msaada wa kibinadamu ndani ya eneo la Gaza, ambayo linaendelea kuzingirwa na mashambulizi ya Israeli toka Oktoba 7 mwaka jana.
Akizungumza katika geti la Rafah, Fidan alilaani machafuko yanayosababishwa na Israeli.
"Muda huu, mita mia chache tu kutoka mahali tunaposimama, janga la kibinadamu linatokea, mauaji ya halaiki yanafanyika," Fidan anasema katika upande wa Misri wa mpaka wa Rafah.
"Watu milioni mbili wamekimbia makazi yao, wanawake na watoto 40,000 wameuawa kishahidi. Hakuna dawa, hakuna chakula, hakuna maji; ndugu na dada zetu wa Kipalestina wanatatizika na njaa katika anga ya wazi.
Kufikia leo, Wapalestina tisa kati ya kumi huko Gaza, takriban watu milioni 1.9, wamelazimika kuyahama makazi yao.
Takriban asilimia 95 ya watu, au watu milioni 2.15, wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula kutokana na mashambulizi ya Israeli.
Akiihutubia jumuiya ya kimataifa, Fidan alihimiza hatua za haraka zichukuliwe: "Ninatoa wito kwa ubinadamu wote. Ikiwa hatutakomesha mauaji haya kwa pamoja, tutashiriki katika mauaji haya kama jamii."
"Kwa hiyo, ni lazima tujitahidi kutoa msaada wote tunaoweza. Ni lazima tuongeze shinikizo kwa Israeli," Fidan alisema.
"Mataifa ya Magharibi, hususani Marekani, lazima yavunje ukimya wao. La sivyo, watakuwa washirika katika mauaji haya ya kimbari," aliongeza.
Wapalestina hawawezi tena kupata matunda na mboga. Mifugo imepunguzwa, na msaada wa chakula hautoshi kukidhi mahitaji.
Hali kadhalika, Fidan alisisitiza utayari wa Uturuki katika kuisaidia Gaza, akisema, "Toka siku ya kwanza ya machafuko, tumefanya kila lililo ndani ya uwezo wetu."
Ziara hiyo inaangazia jukumu kubwa la Uturuki katika kutetea haki za Wapalestina na kuweka msukumo kimataifa katika kukomesha mauaji ya Israeli yanayolenga eneo la Gaza.
Hali katika mfumo wa huduma za afya katika eneo la Gaza ni ya kushtua.
Kati ya hospitali 36, 20 hazina huduma, na 16 hazifanyi kazi.
Kuna upungufu mkubwa wa dawa na vifaa tiba huku magonjwa ya kuambukiza yakienea kwa kasi.