Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan na mwenzake wa Urusi Vladimir Putin wamekutana kujadiliana masuala ya nchi mbili na ya kiulimwengu mjini Astana, mji mkuu wa Kazakhstan, ambapo viongozi mbalimbali wanakutana katika mkutano wa ushirikiano wa Shanghai.
Akiangazia ushirikiano kati ya Uturuki na Urusi, ikiwemo ujenzi wa mtambo wa nyuklia wa Akkuyu siku ya Jumatano, Erdogan alisema, "Tumefanya majadiliano (na Urusi) kuhusiana na mradi wa nyuklia wa Sinop, ni imani yangu kuwa tutachukua hatua madhubuti kuhusu suala hilo.”
Mradi wa Sinop ni mradi pendekezwa katika eneo la Sinop lililopo kwenye ukanda wa Bahari Nyeusi ya Uturuki. Utakuwa ni mradi wa pili wa Nyuklia kwa Uturuki, baada ya ule wa kwanza ulioko kusini mwa Uturuki, na ni mradi wake wa pili unaojengwa kwa ushirikiano na Moscow.
Lengo la kiasi cha biashara
Rais wa Uturuki alionesha imani yake ya kufikia lengo la kiasi cha biashara cha dola bilioni 100, akigusia uwezo wa kuongezeka kwa uhusiano wa nchi mbili.
Putin, kwa upande wake amesema kuwa "licha ya changamoto zilizopo, uhusiano kati ya Urusi na Uturuki unazidi kuimarika, hatua kwa hatua."
Pia aligusia maendeleo katika "miradi ya kimkakati" na kubainisha kuwa idadi kubwa ya watalii, wapatao milioni 6.7 kutoka Urusi walitembelea Uturuki mwaka jana.
Rais wa Uturuki alimkaribisha Putin aweze kuitembelea Uturuki.
Katika majibu yake kwa mwaliko kutoka kwa Erdogan, Putin alisema: "Bila shaka nitakuja."