Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ameelezea wasiwasi wake juu ya kuporomoka kwa imani katika tunu za Ulaya hasa kutokana na bara hilo kushindwa kujibu ukatili wa Israel dhidi ya Gaza.
Akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Ulaya, Mei 9, Rais Erdogan alisisitiza kwamba siku hiyo sio tu inaashiria kuanzishwa kwa umoja wa kisiasa na kiuchumi barani Ulaya bali pia inaheshimu kilele cha juhudi kubwa za pamoja za kutafuta amani.
"Hata hivyo, changamoto mbalimbali kama vile vita, migogoro, vitendo vya kigaidi na mabadiliko ya tabia nchi duniani na katika ukanda wetu vinaathiri bara la Ulaya," amesema Erdogan, kulingana na taarifa iliyotolewa na kurugenzi ya Mawasiliano ya Uturuki siku ya Alhamisi.
Erdogan alisisitiza kuwa baadhi ya taasisi na sera nchini Ulaya zinadharau kile kinachoendelea Gaza, na hivyo kushusha tunu za Ulaya, huku Wapalestina 35,000 wakiwemo watoto 15,000 wakiwa wameuwawa.
"Wakati machafuko, mizozo na vita vinavyoathiri Ulaya na jiografia yetu ya pamoja kubaki bila kutatuliwa, maswali juu ya tunu hizi yataendelea kukua," alionya.
Pia ameongeza kuwa "ongezeko la chuki dhidi ya Uislamu, chuki dhidi ya wageni na ubaguzi wa rangi katika bara zima la ulaya ni tishio kwa watu waishio Ulaya na wahamiaji. Ubaguzi na uhalifu wa chuki dhidi ya Jumuiya ya Uturuki ya Ulaya unazidi kuwa jambo la kawaida."
"Hatua Muhimu"
Katika ujumbe wake, Rais wa Uturuki aliitaka Ulaya kuweka kipaumbele katika sera jumuishi, zenye mwelekeo wa ushirikiano na usawa katika eneo zima la Ulaya na Bonde la Mediterania, akisisitiza umuhimu wao kwa mustakabali wa bara hilo.
"Katika wakati huu muhimu, ambapo kasi ya sera ya upanuzi imeongezeka, ni wakati muafaka kwa nchi yetu na Umoja wa Ulaya kuimarisha ushirikiano katika nyanja zote, ikiwa ni pamoja na mazungumzo ya kujiunga, ambayo ni msingi wa uhusiano wetu, na kuimarisha uhusiano huo," alisema Erdogan.
"Ni muhimu kwa Umoja wa Ulaya kufanya uhusiano wake na nchi yetu kwa nia njema na kwa njia ya haki na yenye mwelekeo wa matokeo, kuepuka sera na maneno ambayo yanazuia uhusiano wetu," aliongeza.
Pia alionya kuwa Uturuki haitosita kutumia nguvu yake ya kimkakati dhidi ya sera gawanyishi zenye kuathiri pande zote.
"Napenda kusisitiza utayari wetu wa kufanya kazi pamoja kwa ajili ya Ulaya yenye mafanikio zaidi, yenye mshikamano, na ya wazi zaidi ambayo nchi yetu inaweza kuchukua nafasi yake. Kwa maneno haya, nawapongeza watu wote wa Ulaya , hasa wananchi wetu kwa siku hii," alisema.