Azerbaijan, taifa ndugu na historia ya uhusiano wa kina na Uturuki imeahidi kuendelea kutoa msaada wake katika kupambana na moto uliozuka kote nchini.
Katika mazungumzo ya simu na mwenzake wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan siku ya Jumamosi, Ilham Aliyev aliwasilisha salamu zake za heri na kuahidi kuwa yuko tayari kuisaidia Uturuki ikiwa ni pamoja na kutumwa kwa ndege ya kuzima moto.
Mazungumzo hayo pia yaliangazia uhusiano wa nchi hizo mbili na maendeleo ya kikanda, kulingana na taarifa kutoka kwa Kurugenzi ya Mawasiliano ya Uturuki.
Erdogan alitoa shukrani zake kwa msaada huo, akisisitiza uhusiano wa kina kati ya mataifa hayo mawili wakati wa nyakati ngumu.
Moto umedhibitiwa
Uturuki imekuwa ikipambana na zaidi ya mioto 70 inayowaka misituni, 69 katika ya hiyo ikiwa imedhibitiwa huku sita ikiwa bado imesalia.
Ripoti za hivi punde kutoka kwa Waziri wa Kilimo na Misitu wa Uturuki Ibrahim Yumakli zilionesha kuwa nguvu ya moto wa msitu katika jimbo la Izmir magharibi mwa Uturuki imepunguzwa, bila tishio la haraka kwa jiji hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Izmir, amewahakikishia kuwa hali ya sasa ilikuwa shwari na hapakuwa na sababu ya kuomba msaada wa kimataifa.
Azerbaijan imekuwa ikijitolea kuisaidia Uturuki ambapo hapo awali, ilisaidia katika utafutaji na uokoaji, pamoja na juhudi za kujenga upya, wakati matetemeko ya ardhi yenye ukubwa wa 7.7 na 7.6 yaliyoikumba Uturuki mnamo Februari 6, 2023 na kuuwa zaidi ya watu 53,000.
"Kama vile Uturuki inavyosimama na Azerbaijan nyakati za furaha na huzuni, sisi daima tunasimama karibu na Uturuki na tutaendelea kufanya hivyo. Kwa sababu sisi ni taifa moja, mataifa mawili,” alisema Aliyev mapema mwaka huu, kabla ya maadhimisho ya mwaka wa kwanza wa matetemeko makubwa ya ardhi yaliyotokea kusini mwa Uturuki.