Rais wa uturuki Recep Tayyip Erdogan amempokea mkuu wa Usalama wa Taifa wa Poland Jacek Siewiera na mshauri wa Usalama wa Taifa wa Romania Ion Oprisor, mjini Ankara.
Mkutano huo uliofanyika katika ikulu ya Rais siku ya Jumatano, ulizungumzia kuimarisha ushirikiano kati ya mataifa, vita vya Ukraine, pamoja na hali ya hivi karibuni katika mzozo wa Israeli na Palestina; kurugenzi ya mawasiliano ya Uturuki ilisema kupitia mtandao wa X.
Rais Erdogan amesema kuwa mbinu ya Ankara kuhusu Ukraine inalingana na Poland na Romania, na kwamba maendeleo hayajafanywa katika kufanikisha amani licha ya zaidi ya miaka miwili ya migogoro endelevu.
Akisisitiza haja ya kufungua mlango utakaotoa njia ya heshima kwa pande zote mbili, Erdogan alisema mipango ya amani ya upande mmoja ambayo haihusishi Urusi " ina nafasi dhaifu ya kufanikiwa.”
Rais Erdogan amesema gharama za vitendo vya Israel kule Gaza ni kubwa, akiongeza kuwa matukio hayo hayawakilishi tu mtihani wa usalama bali pia mtihani wa kibinadamu.
Kiongozi huyo wa Uturuki amesema Israel imezidisha kiwango cha "mauaji" licha ya idhini ya Hamas ya kusitisha mapigano, akisisitiza kwamba kanuni na sheria zinazotumika kuitetea Ukraine, zitumike kwa Gaza pia.
Kulingana na kurugenzi ya mawasiliano ya Uturuki, Rais Erdogan amesema kuwa Uturuki inatarajia mshikamano kamili ndani ya NATO, akiwataka washirika kujizuia kuwekeana vizuizi, na kuachana na juhudi za kuitenga Ankara katika muktadha wa ushirikiano wa NATO na Umoja wa Ulaya
Mkurugenzi wa mawasiliano Fahrettin Altun, mshauri mkuu wa Rais Erdogan Akif Cagatay Kilic, na maafisa wengine pia walihudhuria mkutano huo.