Japo walijua kuwa hawaendi kokote hata wakishinda, Zambia waliingia uwanjani ulimi nje wakihemea japo ushindi mmoja.
Nao naam, ulimwengu uliwaitikia ombi lao maana chini ya dakika tatu za mwanzo walitikisa nyavu ya Costa Rica kupitia Lushomo Mweemba alivvyopokea kutoka Kona wa Adel Chitundu.
Baada ya hapo mechi iliingia ghafla gia ya tano maana mbio kutoka pande zote mbili ilishika kasi huku La Ticas wakitafuta kusawazisha ili kurudisha mizani sawa.
Lakini Wapi! Copper Queens walikuwa kama vile wamewashwa moto ndio mwanzo walipepeta na kudana na kuwahemesha Costa Rica.
Kufikia dakika ya 30' Kapteni aliwaonyesha kwanini yeye ndiye Kapteni.
Barbara Banda alisukuma uvunguni bao lake la kwanza katika shindano hilo, ambalo limetajwa pia kuwa bao la 1000 katika shindano zima tangu kuzinduliwa.
Costa Rica nao walipata njia ya kufuta aibu usoni mara tu baada ya mapumziko, huku Melissa Herrera akijibu kwa haraka na kupiga shuti la karibu baada ya Valeria Del Campo kuupiga mpira kwa kichwa kutoka kwenye mstari wa goli.
Costa walionekana kupata motisha lakini Copper Queens wakawana nao ndio hawaambiliki hawashikiki.
Bao la Lala salama, la Rachael Kundananji katika muda wa ziada uliwafungia kesi Zambia kwa ushindi wa 3-1 na kipenga cha kumalizika pambano lilipokewa kwa shangwe na nderemo kutoka kwa mashabiki wa Zambia waliokuwepo uwanjani wakijua kuwa japo wanaondoka, wanaondoka kichwa juu.
Zambia na Costa Rica wako nje sasa wakiwapisha Japan na Uhispania ambao ndio wanaosonga mbele sasa kwa kushikilia uongozi wa Kundi C.