Kwa mara ya kwanza, Wekundu wa Msimbazi walitumia jezi hizo watakazovaa msimu ujao, katika mechi yake ya kirafiki huku wakiendelea na kambi yao ya mazoezi.
Sare hizo zimeweka historia kwani zilitambulishwa kwenye kilele cha mlima Kilimajaro siku chache zilizopita na kuifanya klabu ya Simba kuwa timu ya kwanza kufanya uzinduzi wa aina hiyo.
Hatua hiyo ya Simba kufanya uzinduzi wa jezi yake kwenye kilele cha mlima mrefu zaidi barani Afrika, kilifuatwa na mapokezi ya kibegi hicho kilichofanywa na Waziri wa Habari nchini Tanzania Nape Nnauye huku mashabiki wa Simba kutoka eneo la Kilimanjaro wakijitokeza.
Jezi za kwanza za timu hiyo zilizinduliwa zikiwa na majina ya viongozi wa Tanzania wakiongozwa na Mama Samia Suluhu Hassan, Kassim Majaliwa, Husssein Mwinyi, Philip Mpango, Rais wa heshima wa Simba Mohammed Dewji, na Spika wa bunge Tulia Ackson.
Simba imeeleeza kuwa jezi zenye majina ya viongozi hao zitapigwa mnada na pesa hizo kutumika kwenye ujenzi wa wodi ya afya za kina mama katika vituo vya afya vikiwemo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na Zanzibar. Aidha, imeahidi kutoa zawadi kwa wahusika walioshiriki katika uzinduzi wa jezi hiyo mlima Kilimanjaro.
Simba wako tayari Kunguruma msimu huu
Klabu ya Simba imewahakikishia mashabiki kuwa kambi yake ya maandilizi nchini Uturuki imekuwa yenye mafanikio huku wakisalia na siku chache kabla hawajarudi nyumbani Tanzania.
Miamba hao, wanaoongozwa na Kocha Mkuu Roberto Oliviera ‘Robertinho’, walitua Uturuki mapema mwezi huu huku kikosi hicho kikiwajumuisha wachezaji na wakufunzi wapya kwenye benchi lake la kiufundi waliotinga katika timu hiyo msimu huu.
Aidha, Simba imeeleza kukamilisha shughuli zake katika dirisha hili la uhamisho na kuridhiswa na shughuli zake za kuwa na wachezaji bora watakaoiletea ubingwa msimu huu.
Mchezaji wa mwisho kutua kambini kwenye timu hiyo ni Luis Miquissone baada ya wenzake Shaban Chilunda, Abdallah Hamisi, na Hussein Kazi pia kuwasili Uturuki.
Aidha, Simba inatarajiwa kurejea Tanzania wiki ijayo kushiriki wiki ya Simba itakayozinduliwa siku ya Jumamosi na kumalizika tarehe 6 Agosti.