Baada ya mechi ya Jumapili Mazembe watasafiri Tunis kwa mechi ya marudio ili kujua atakayefuzu nusu fainali / Picha: X -  TP Mazembe 

Ngoma imepata mpigaji. Wakata viuno wa Jamhuri ya Demokrasia ya Congo TP Mazembe watawachezesha wakinzani wao kutoka Tunisia uwanjani Dar, kwa mechi ya tatu ya robo fainali ya kombe la ligi ya Afrika.

TP Mazembe watakuwa wanatafuta kulipiza kisasi maana mara ya mwisho kukutana na Esperance ya Tunisia ilikuwa nusu fainali ya CAF klabu bingwa Afrika, ambapo Esperance iliwabandua kwa jumla ya magoli.

Japo wanachezea uwanja wa kuazima kwa majirani zao Tanzania, kocha wa Mazembe Lamine N’Diaye anasema halijawavunja moyo kwani wamejiandaa kwa mapambano popote pale.

"Espérance sio timu inayohitaji utambulihso. Timu hizi mbili zina historia nzuri na upinzani wao huwa mkubwa kila wakati. Esperance wana timu nzuri, Lakini Mazembe pia tuko sawa. Tutapambana.'' Alisema kocha Lamine.

Mazembe wanachezea mechi zao za nyumbani jijini Dar es Salaam, baada ya kushindwa kupata vibali muhimu kurejea Lubumbashi lakini matumaini yao ni kuwa Wakongomani walioko Dar watajitokeza kuwapigia upatu.

Wakati huo huo, kocha mkuu wa Esperance Tarek Thabet anaamini halitakuwa pambano rahisi timu itakaposhuka dimbani dhidi ya TP Mazembe DRC.

“Tumejiandaa vizuri sana na tayari kwa changamoto. Tunajua haitakuwa rahisi kwa sababu tunacheza dhidi ya timu nzuri sana,'' alisema kocha Tarek. ''Mazembe ina uzoefu mkubwa na pia tunakabiliwa na timu ambayo inaimarika sana,” mtaalamu huyo aliongezea.

Hii ni mechi yao ya ufunguzi kwa maana kuwa kutakuwa namechi ya marudio mjini Tunis baada ya hapa.

TRT Afrika