Suarez pia aliiwezesha Uruguay kutwaa taji la Copa America, mnamo 2011. / Picha: AFP
Adhabu inawasubiri mabeki wa ligi ya MLS Marekani baada ya Inter Miami kutangaza kumsaini Luis Suarez kuungana na nyota mwenza wa Barcelona zamani, Lionel Messi.

Mshambuliaji huyo wa Uruguay alifunga mabao 195 na kuongeza pasi za magoli 113 katika mechi 283 akiichezea Barcelona.

Mbali na Messi, Suarez atajiunga na wachezaji wenzake wa zamani wa Barcelona Sergio Busquets na Jordi Alba waliotua timu hiyo maarufu ya Miami.

Licha ya umri wake, Luis Suarez alitunukiwa mchezaji bora na mshambuliaji bora katika ligi ya Brazil msimu uliopita akiichezea Gremio, kwa kufunga mabao 26 na kuweka pasi 17 katika mechi 53.

Nyota wa zamani wa England na Manchester United David beckham, mmiliki mwenza wa Inter Miami, alifurahia sana kumsajili Suarez.

"Tunafurahi kuwa na mchezaji wa ubora wa Suarez na shauku ya mchezo kujiunga na klabu yetu," Beckham alisema. "Anajiunga na kikosi ambacho kinahamasisha kizazi kijacho na tunatarajia kumwona akiingia uwanjani."

Inter Miami ikimtambulisha Luis Suarez. Picha: Luis Suarez

"Tunafurahi kumkaribisha Mshambuliaji wa kiwango cha ulimwengu Luis Suarez kwenye kilabu yetu," mmiliki mkuu wa Inter Miami Jorge Mas alisema. "Luis ni mshindani mkali ambaye ari yake ya kushinda inajumuisha kile tunachotaka kutoka kwa wachezaji wetu."

Suarez, ambaye atatimiza miaka 37 mwezi ujao, alishinda mataji manne yakiwemo Liga na Ligi ya Mabingwa Champions League na Barcelona na pia akakusanya mataji ya ligi na Ajax na Atletico nchini Uhispania.

Nyota huyo wa Uruguay ambaye alitamba alipokuwa Gremio, Barcelona, Liverpool, Atletico Madrid na Ajax, atajiunga na Inter Miami kwa msimu wa 2024, klabu ya MLS ilitangaza Ijumaa.

"Ninafurahi sana na ninafurahi kuchukua changamoto hii mpya na Inter Miami," Suarez alisema. "Siwezi kusubiri kuanza na niko tayari kufanya bidii ili nifanikishe ndoto ya kushinda mataji zaidi na klabu hii kubwa, kuwa ukweli.

"Nina matumaini juu ya kile tunachoweza kukifikia pamoja na matamanio yetu ya pamoja. Nitajitolea nguvu zangu ili kuleta furaha kwa mashabiki hawa wakuu ambao nimesikia mengi wakati nitakapovaa rangi za Inter Miami na ninatarajia kuungana tena na marafiki na wachezaji wakubwa."

Suarez pia aliiwezesha Uruguay kutwaa taji la Copa America, mnamo 2011.

TRT Afrika na mashirika ya habari