Simba Wahindi ngao ya jamii | Picha: Simba Twitter

Tamati ya mashindano ya kombe la Ngao ya Jamii iliwapa fursa mashabiki wa soka Tanzania na duniani kote ya kutazama mechi ya watani wa jadi (Derby) kati ya Simba SC na Yanga SC.

Matokeo yaliisha kwa Simba SC kushinda kwa penalti 3-1 na kujinyakulia kikombe cha ngao ya jamii hivyo kuendeleza ubabe wa kuifunga Yanga SC mara mbili mfululizo.

Katika dakika 45 za mwanzo mchezo ulikuwa wa kuvutana kila timu ikijitahidi kucheza mpira wa kutandaza pasi na kujilinda licha ya mashambulizi kadhaa kufanyika.

Hali iliendelea hivyo mpaka mwamuzi alipopuliza kipenga cha mwisho dakika 90 za mchezo hazikuweza kumjua mshindi. Ndipo mikwaju ya penalti ikaingilia kati na kuamua nani atakuwa bingwa wa Ngao ya Jamii na kuanzisha safari ya msimu wa ligi mpya.

Golikipa shujaa wa mechi

Penalti hazina fundi, iwe mpigaji au kipa ndivyo mashabiki wengi husema kila upigaji wa matuta unapowadia kwenye mechi fulani. Ally Salim mlinda mlango wa Simba SC aliibuka shujaa wa mchezo baada ya kupangua penalti 3 za wapigaji wa Yanga SC.

Kipa wa Simba Ally Salim akidaka penalti | Picha: Simba sc

Kama ilivyo nadharia ya penalti timu iliyocheza vizuri zaidi hupoteza mchezo hicho ndicho kilichotokea kwa Yanga SC. Walisifika kwa kucheza vizuri lakini walishindwa kuitumia vyema mikwaju ya penalti.

Azam mshindi wa tatu Katika mechi iliyozikutanisha Azam FC na Singida Fountain Gate FC kutafuta mshindi wa tatu, Azam FC waliibuka washindi kwa bao 1-0 na kuwa mshindi wa tatu wa mashindano.

TRT Afrika