Simba FC

''Jiji la Daresalaam limesimama,'' ndio kauli ya kila mmtu unayezungumza naye kutoka huko.

Wekundu wa Simba umetapakaa huku msisimko ukijitokeza wazi miongoni mwa maelfu ya mashabiki wanaoonekana wakitiririka uwanja wa Benjamin Mkapa.

''Ni siku moja ambayo mashabiki wa Simba wa hapa Tanzania na hata kimataifa wanakuja kusherehekea uwepo wa klabu yao,'' anasema Salim Kikeke, mtangazaji nguli wa michezo na shabiki namba moja wa Simba FC.'' ''Vile vile ni nafasi ya kuona wachezaji wapya waliosajiliwa na klabu.'' anaonegeza Salim.

Zaidi ya mashabiki 60 000 wa SImba wamemiminika uwanja wa Benjamin Mkapa kujionea kikosi chao kipya Picha : Salim Kikeke

Katika kusherehekea siku hii, Simba FC imeandaa mechi murwa na Power Dynamos wa Zambia ikiwa ndio mara ya pili wanakutana na klabu hiyo. Hii ni mechi ya 15 ya maadhimisho ya Simba Day tangu kuzinduliwa kwake.

Mbali na kuzinduliwa kwa kikosi na jezi zake mpya na mechi ya Simba na Dynamo, mama wa taifa Dr Samia Suluhu Hassan amethibitisha kuhudhuria hafla ya leo na hivyo kuipatia klabu hiyo haki ya kujigamba kama mojawapo ya klabu tajika sio ndani ya nchi pekee bali na nje pia.

Ligi ya Tanzania ni miongoni mwa ligi kubwa zaidi barani Afrika ikikumbukwa kuwa Yanga ya Tanzania walikosa kwa unyoya tu kunyakua ubingwa wa Kombe la shirikisho CAF walipikia fainali na kupoteza kwa Algeria.

Licha ya kuwa misimu miwili iliyopita Simba SC haikufanya vyema sana katika mitanange ya bara, wanamsimbazi kama wanavyo jiita mashabiki wake wamepata jeki kubwa na kuamini kuwa usajili mpya waliopata utaipeleka klabu hiyo hadi kileleni bila tashwishi.

Ilianzishwa mwaka 1936 kama Sunderland na mwaka wa 1971 hatimaye ikabadilishwa jina na kuitwa Simba. / Picha : Twitter Simba SC 

“Ni siku muhimu kwa Wanasimba wote, wanataka kuja kuiona timu yao. Na niwahakikishie tuna tima imara msimu huu,'' amesema kocha wa Simba Roberto Oliviera ‘Robertinho’

''Unajua kila timu inakuwa na msimu mzuri na msimu mbaya, kwahiyo Simba nadhani haikupata msimu mzuri uliopita na hata msimu uliotangulia pia haukua mzuri sana.'' anasema Salim. ''Lakini ukitazama jinsi usajili ulivyofanywa na mwelekeo wa timu na meneja mpya, kun amatumaini kwamba msimu huu utakuwa wa Simba/'' anaongeza.

Miongoni mwa wasajili wapya wa Simba SC ni :

  • Willy Essomba Onana - Mshambuliaji - Kutoka Rayon Sport
  • Che Fondoh Malone - Beki - Kutoka Cotton Sport Club
  • David Kameta - Beki - Kutoka Mtibwa Sugar
  • Aubin Kramo - Mshambuliaji - Kutoka Asec Mimosa
  • Fabrice Ngoma - Kiungo cha kati - Kutoka Al Hilal Sudan
  • Abdallah Hamisi - Kiungo cha kati - Kutoka Bandari FC
  • Shaban Iddi Chilunda - Mshambuliaji - Kutoka Azam FC

Miongoni mwa wasajili wapya ni Che Fondoh Malone ambaye amesajiliwa kutoka Cotton Sports ya Cameroon. Likuwepo naye mjini Istanbul baada ya usajili kwa kambi y akupigwa msasa ambayo ilihusisha mazoezi maalum na ukufunzi wa hali ya juu kama maamndalizi.

Che Fondoh anasema Simba ni moja ya timu kubwa Afrika hivyo kila mchezaji angependa kuitumikia na kuwa atajitolea kikamilifu kuwaonesha Watanzania katika mechi dhidi ya Dynamo, kionjo kwa nini yeye ni beki nyota.

Simba SC imeshinda mataji 22 ya ligi na vikombe vitano vya kombe la FA Tanzania,  / Picha : Twitter Simba SC 

Ilianzishwa mwaka 1936 kama Sunderland na mwaka wa 1971 hatimaye ikabadilishwa jina na kuitwa Simba.

Simba SC imeshinda mataji 22 ya ligi na vikombe vitano vya kombe la FA Tanzania, na imeshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika mara nyingi. Pia ni miongoni mwa vilabu vigogo Afrika Mashariki na Kati, baada ya kutwaa Ubingwa wa Klabu Bingwa ya CECAFA mara sita.

''Simba haijapata jina la kuitwa Simba wa mataifa bure.'' Anasema Salim Kikeke. '' imepata jina hilo kutokana na mafanikio makubwa kimataifa. Najua watani wetu walicheza fainali msimu uliopita lakini simba ukitizama ndio iliyopata mafanikio makubwa zaidi kimataifa na hata nyumbani.'' Anasifia Salim.

Kwa sasa Simba imeorodheshwa klabu ya 7 barani Afrika na shirikisho la soka CAF.

TRT Afrika