Katika siku ya ajabu ya mbio za marathon, nyota wa Uholanzi Sifan Hassan amechupa hadi nambari ya pili kwenye orodha ya wanawake bora kwenye mbio hizo baada ya kukimbia muda wa saa mbili na dakika 13 na sekunde 44 (2:13:44) na kushinda mbio hizo za Chicago.
Ushindi huo wa bingwa huyo wa medali ya dhahabu ya Olimpiki Sifan, ulimnyima Mkenya Ruth Chepngetich taji lake la tatu mfululizo katika mbio za masafa marefu za Chicago siku ya Jumapili.
"Nilikimbia sana. Nina furaha," Sifan alisema. "Nilikimbia wakati wa kushangaza. Sikuwahi kufikiria ningekimbia muda huu. Ni ajabu. Ni ajabu." Sifan alisema.
Sifan Hassan mwenye umri wa miaka 30, alikimbia kasi ya pili zaidi katika historia ya mbio za marathon za wanawake – duniani iki pia ni mbio yake ya pili ya marathon.
Rekodi hii ya mkimbiaji huyo mzaliwa wa Ethiopia inatanguliwa tu na rekodi ya dunia ya wanawake ya Tigist Assefa aliyekimbia muda wa 2:11:53 katika mbio za Berlin mwezi uliopita.
""Ninaipenda tu. Maumivu na wakati ni mzito sana lakini pindi ukimaliza unataka kurudia tena. Ninaipenda. Ni ajabu. Siwezi kuelezea," Sifan alifafanua.
Ruth Chepngetich wa Kenya, ambaye alikuwa akisaka taji la tatu mfululizo la wanawake, alimaliza wa pili kwa 2:15:37 huku naye Megertu Alemu wa Ethiopia akimaliza wa tatu kwa muda wa 2:17:09 naye Mkenya mwingine Joyciline Jepkosgei, bingwa wa mbio za New York Marathon 2019 na London Marathon 2021 akitoka wa nne kwa muda wa 2:17:23.
Orodha kamili ya matokeo mbio za Chicago Marathon 2023 kwa wanawake
- Sifan Hassan (NED) 2:13:44
- Ruth Chepngetich (KEN) 2:15:37
- Megertu Alemu (ETH) 2:17:09
- Joyciline Jepkosgei (KEN) 2:17:23
- Tadu Teshome Nare (ETH) 2:20:04
- Genzebe Dibaba (ETH) 2:21:47
- Emily Sisson (USA) 2:22:09
- Molly Seidel (USA) 2:23:07
- Rose Harvey (GBR) 2:23:21
- Sara Vaughn (USA) 2:23:24