Kenya, ikiwa mojawapo ya mataifa ya Afrika yanayopigiwa upatu kwenye mashindano yajayo ya Riadha duniani, Budapest, inasema kuwa iko tayari kwa mapambano hayo yatakayoanza tarehe 19 mwezi huu.
Kenya imetangaza kikosi cha wachezaji 56 kitakachoongozwa na Emily Ngii, ambaye ni mshindi wa medali ya shaba katika mbio za mita 10,000 kitengo cha wanawake mwaka uliopita wakati wa mashindano ya Jumuiya ya Madola, Birmingham, Uingereza.
Ngii, mwenye umti wa miaka 36, ametangazwa kuwa nahodha wa timu hiyo, kutokana na uzoefu wake wa kuwa kikosini kwa muda mrefu ambapo huku akisadiwa na Julius Yego.
Mkufunzi wa timu hiyo David Letting, ametangaza kikosi chenye wanariadha 56, wakiwemo wanariadha 32 wa kiume na 24 wa kike.
"Kila mwanariadha atakayekuwa Budapest, analenga kutwaa tu ubingwa na tunaelekea vitani. Ombi letu ni kufanikiwa pakubwa na wanariadha wetu wote wako tayari kujizolea ubingwa." Kocha Letting alisema.
Matumaini ya Kenya yatakuwa kwa kitengo cha mbio za mita 1,500, na mita 5,000 huku wakimtegemea weledi wa mbio hizo, Faith Kipyegon anayeshikilia rekodi ya dunia. Wakati huo, shirikisho la Riadha likiongozwa na Rais Jackson Tuwei limweka imani kwa mkimbiaji wa mita 100, Ferdinand Omanyala.
Rekodi za Dunia alizoweka msimu huu Faith Kipyegon, mbio za mita 1500, na mita 5000 kwa wanawake, zimeidhinishwa na shirikisho la riadha duniani. Faith alikimbia muda wa 3:49.11 mjini Florence tarehe 2 Juni 2023 na kuweka rekodi ya dunia ya mita 1500.
Aidha, mnamo Juni 9, 2023, Kipyegon alikimbia muda wa 14:05.20 mjini Paris na kuweka rekodi ya dunia ya mbio za mita 5000.
Timu ya Kenya kwenye mashindano ya Budapest 2023 inaendelea na maandalizi yake katika kambi ya makazi ya timu, katika uwanja wa Michezo wa Kimataifa Moi Kasarani, Nairobi kabla ya onyesho la kimataifa linalotarajiwa kufanyika Agosti 19-27 nchini Hungary.