Shirikisho la Soka la Saudi Arabia limewasilisha barua rasmi ya nia ya kutoa zabuni ya kuandaa kombe la Dunia la FIFA 2034

Siku chache tu baada ya Saudi arabia kutangaza nia yake ya kutoa zabuni ya kuwa mwenyeji wa kombe la dunia la soka 2034, Oktoba 4, rais wa shirikisho la soka la Saudi Arabia (SAFF) Yasser Al Misehal ameandika barua rasmi kwa FIFA kuendeleza juhudi hizo.

''Shirikisho la Soka la Saudi Arabia (SAFF) limewasilisha barua ya kufafanua nia (LOI) na kusaini tamko kwa FIFA ili kuwasilisha zabuni ya kuwa mwenyeji wa Kombe la dunia la FIFA la 2034,'' imesema taarifa.

Barua hiyo ya dhamira inathibitisha rasmi kujitolea kwa Ufalme huo wa Kiarabu kuanza mchakato wa zabuni uliowekwa na FIFA.

Saudi Arabia, kupitia taarifa rasmi iliyotolewa na Shirikisho la Soka la Saudi Arabia (SAFF), inasema kuwa nia yake ni kuchagia ukuaji wa mpira wa mguu nje na ndani ya nchi hiyo.

Wiki iliyopita tulitangaza matamanio yetu ya kuandaa kombe la Dunia la FIFA ™ la 2034, na uwasilishaji huu rasmi unaendelea na safari yetu ya kufanya ndoto za watu wetu kuwa ukweli. Kombe la Dunia la FIFA la 2034 ni mwaliko wetu kwa ulimwengu kushuhudia maendeleo ya Saudi Arabia, uzoefu wa utamaduni wake na kuwa sehemu ya historia yake.

Rais wa SAFF, Yasser Al Misehal

Dhamira ya Saudi Arabia kutoa zabuni ya Kombe la dunia la FIFA la 2034 ni ya kwanza ya kihistoria na inaonyesha malengo ya taifa hilo ya kufungua fursa mpya za mpira wa miguu katika ngazi zote na kujitolea kusaidia ukuaji wa mchezo huo katika pembe zote za ulimwengu.

Saudi arabia inasema kuwa zabuni hiyo yake imeungwa mkono na zaidi ya mashirika 70 ya wanachama wa FIFA kutoka mabara tofauti ambayo yameahidi hadharani kuunga mkono chini ya saa 72 baada YA SAFF kutangaza nia yake ya kuwasilisha zabuni ya Kombe la Dunia la Fifa ™

Wiki iliyopita, FIFA iliweka tarehe 31 Oktoba kama siku ya mwisho kwa mashirikisho kuelezea rasmi nia ya kutoa zabuni na Novemba 30 kurudisha makubaliano ya kisheria yaliyotiwa saini ambayo yanahitaji uungwaji wa serikali za kitaifa.

TRT Afrika na mashirika ya habari