Timu ya taifa ya soka ya Rwanda

Shirikisho la Soka Rwanda (FERWAFA) limemteua Torsten Frank Spittler kuwa kocha mpya wa timu ya taifa.

FERWAFA inafurahia kutangaza kwamba Torsten Spittler Frank (61) ameteuliwa kuwa kocha mkuu mpya wa timu ya taifa ya wanaume ya Rwanda, " ilisema taarifa ya shirikisho la Soka la Rwanda FERWAFA iliyotolewa Jumatano.

Spittler, mmiliki wa leseni ya kiwango cha Uefa Pro anachukua nafasi ya kocha aliyeondoka Carlos Ferrer ambaye alitengana na timu mwezi Agosti mwaka huu baada ya kushindwa kusaidia Amavubi Stars kufuzu kwa Kombe la mataifa ya Afrika (AFCON) 2023.

Spittler sasa ni mjerumani wa tano kuiongoza timu ya Taifa ya soka ya Rwanda baada ya Otto Pfister (1972 -76), Rudi Gutendorf (1999-2000), Michael Nees (2006-2007) na Antoine Hey (2017-2018).

Kocha huyo mpya Torsten Frank Spittler anatarajiwa kuiandaa timu hiyo kwa mechi za kufuzu kwa kombe la dunia la FIFA 2026.

Rwanda imewekwa Katika Kundi C la kufuzu Kombe la Dunia la FIFA 2026.

Amavubi Stars watafungua kampeni yao ya kufuzu kombe hilo dhidi ya Zimbabwe na baadaye kumenyana na Afrika kusini Novemba hii.

Rwanda iko kwenye kundi moja pia na Super Eagles ya Nigeria, Benin na Lesotho.

Spittler ana uzoefu wa kutosha ikiwa pamoja na kuifunza klabu ya ligi ya Ujerumani Bundesliga, 1960 Munich mwaka 1993.

Kocha huyo pia ana uzoefu wa kuziongoza timu za Afrika. Alikuwa mkufunzi mkuu Sierra Leone mwaka 2025 na alikuwa mkurugenzi wa kiufundi wa shirikisho la soka la Msumbiji kutoka 2029 hadi 2011.

TRT Afrika