Real Madrid wakisherehekea ubingwa wao baada ya kuifunga Pachuca ya Mexico kwa mabao 3-0./Picha: CalmViJR

Real Madrid imetwaa ubingwa wa Kombe la FIFA Intercontinental.

Mabingwa hao kihistoria wa Ligi ya Mabingwa Ulaya wametwaa Kombe hilo siku ya Disemba 18 katika mchezo wa fainali dhidi ya Pachuca ya nchini Mexico.

Mchezo huo uliofanyika katika uwanja wa Lusail nchini Qatar, ulishuhudia mabao ya miamba hao wa Hispania yakitiwa nyavuni na Kylian Mbappé, Rodrygo na Vinicius Junior.

Ushindi huo wa mabingwa hao Hispania dhidi ya Pachuca ya nchini Mexico, umempa kocha Carlo Ancelotti nafasi kuweka rekodi ya kuwa kocha mwenye mafanikio mengi ndani ya Santiago Bernabéu, akiwa na mataji 15.

Kabla ya hapo, mtaliano huyo alikuwa sawa na gwiji mwingine wa klabu hiyo Miguel Muñoz, ambaye aliwahi kuifundisha Real Madrid kwenye miaka ya 60 na 70.

Kwa upande wake, kiungo na nahodha wa klabu hiyo Luka Modric, ameingia kwenye vitabu vya historia ndani ya Real Madrid akiwa amejishindia taji lake la 28, tangu ajiunge nao mwaka 2012.

Pata habari zaidi kupitia Whatsapp channels

TRT Afrika