Mabingwa wa kihistoria wa Ligi ya Mabingwa Ulaya (UEFA) Real Madrid ya Hispania, wameendeleza ubabe wao kwenye michuano hiyo mikubwa Ulaya baada ya kuifunga Borussia Dortmund ya Ujerumani mabao 5-2.
Hata hivyo, iliwalazimu vigogo hao wa Ulaya kuzinduka katika kipindi cha pili, baada ya Borussia Dortmund kutangulia kufunga mabao mawili kupitia kwa Donyell Malen na Jamie Gittens, katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya uliofanyika Oktoba 22 kwenye uwanja wa Santiago Bernabeu.
Vinicius Junior aliibuka nyota wa mchezo huo baada ya kutupia kambani mabao 3, huku mengine mawili yakiwekwa kimiani na mabeki Antonio Rudiger na Lucas Vazquez.
Vijana wa Carlo Ancelotti hawakuamini lililokuwa linatokea hadi kumalizika kwa dakika 45 za kwanza za mchezo huo wa Ligi ya Mabingwa ya Ulaya, baada ya kuruhusu mabao mawili ndani ya uwanja wa nyumbani uliokuwa umefurika mashabiki.
Hata hivyo, mabingwa hao wa mara 15 wa michuano hiyo mikubwa Ulaya, walizinduka katika kipindi cha pili, wakiwa na hofu ya kupoteza mchezo wa pili kati ya mitatu waliocheza hadi sasa, na kuzawazisha mabao mawili, kabla ya kuongeza mengine matatu.
Mabao mawili yaliyofungwa ndani ya dakika mbili na Antonio Rudiger na Vinicius Junior, yaliirudisha Real Madrid mchezoni, na safari ya kupindua meza ndani ya Santiago Bernabeu ikaanza.
Timu hizo zilikutana mara ya mwisho kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya iliyofanyika Juni 1, 2024 kwenye uwanja wa Wembley, ambapo Real Madrid iliifunga Borussia Dortmund mabao 2-0, na kutawazwa kama mabingwa wa Ulaya kwa ya 15, katika historia ya klabu hiyo.