Na Edward Qorro
TRT Afrika, Istanbul, Uturuki
Unaweza kuiita El Clásico ya kufungulia mwaka.
Ndio; Real Madrid na Barcelona zitapimana ubavu katika mchezo wa fainali ya Supercopa de España utakaofanyika Januari 12, katika uwanja wa Mfalme Abdullah jijini Jeddah, Saudi Arabia.
Miamba hao wawili kutoka nchini Hispania watakutana katika mtanange huo baada ya kushinda michezo yao ya awali ya mashindano hayo ambayo yalishirikisha timu nne.
Ikumbukwe kuwa, Barcelona ndio ilikuwa ya kwanza kujikatia tiketi ya kucheza fainali ya Supercopa de España baada ya kuifunga Athletic Bilbao ya nchini Hispania kwa mabao 2-0, siku ya Januari 8.
Mabao hayo yalitiwa kimiani na Gavi na Lamine Yamal.
Siku iliyofuata, Real Madrid walikuwa na kibarua kizito cha kukabiliana na Real Mallorca, ambapo iliwabidi mabingwa hao wa kihistoria wa Ligi ya Mabingwa Ulaya kusubiri mpaka kipindi cha pili kuanza kufunga kwenye mchezo huo.
Real Madrid ilijipatia magoli yake kupitia kwa Jude Bellingham, bao la kujifunga la Martin Valjent kabla karamu ya mabao haijahitimishwa na Mbrazil Rodrygo Goes, katika mchezo ambao ulishuhudia vurugu baada ya filimbi ya mwisho.
Supercopa de España ni nini?
Yakiwa yameanzishwa mwaka 1982, mashindano ya Supercopa de España, yalianza kwa kushirikisha timu mbili kutoka Hispania.
Hata hivyo, kuanzia mwaka 2020, mfumo wa mashindano hayo ulibadilika na kuanza kushirikisha timu nne; ambazo ni bingwa wa Ligi Kuu ya Hispania maarufu kama La Liga na mshindi wa pili wa ligi hiyo, pamoja na bingwa wa Kombe la Mfalme, maarufu kama Copa del Rey pamoja mshindi wa pili wa michuano hiyo.
Real Madrid ndio mabingwa watetezi wa Supercopa de España kwa sasa baada ya kuwafunga mahasimu wao Barcelona kwa mabao 4-1 katika mchezo uliofanyika jijini Riyadh, Saudi Arabia mwaka 2024.
Hata hivyo, Barcelona ndio klabu iliyoshinda taji hilo mara nyingi zaidi, ikiwa imelinyakua kombe hilo mara 14, ikifuatiwa na Real Madrid ambaye imeshinda mara 13.