Ferdinand Omanyala anasema Olimpiki iliyopita alikuwa chipukizi, lakini 2024 anakuja kama jina kubwa mwenye malengo makubwa zaidi/ Picha : TRT Afrika

Na Lynne Wachira

TRT Afrika, Nairobi Kenya

''Mazoezi sio kitu rahisi. Kuna watu wanadhania kabla ya shindano huwa tumeketi kula raha, maandalizi ni makubwa mno.''

Maneno ya Ferdinand Omanyala. Mwanariadha anayesifiwa kuwa mwenye kasi zaidi Afrika. Na Uswahilini msemo ni 'Ukiona vyaelea jua vimeundwa'.

Hakuna shaka hili ni tangazo rasmi la Omanyala kuwa ameingia katika 'full gear' katika maandalizi yake ya mwaka 2024.

Anacho lenga zaidi Omanyala mwakani ni mashindano ya Olimpiki mjini Paris Ufaransa.

''Mwakani lengo langu kubwa ni kushinda shindano la Olimpiki. Wakati ule mwingine niliingia Olimpiki kama chipukizi lakini sasa naingia kama mmoja wanaopigiwa upatu kushinda,'' Omanyala anaambia TRT Afrika.

Mabadiliko makubwa

Ferdinand Omanyala na kocha wake wameelezea kutoshiriki baadhi ya mashindano ya mwaka 2024 ili kujipa muda zaidi wa maandalizi kwa mashindano makubwa kama Olimpiki na Diamond league / Picha - Omanyala 

Ndoto kubwa ya Ferdinand Omanyala msimu huu ilikuwa kuandikisha historia kama mwanaraidha wa kwanza kutoka Afrika, kutwaa ushindi katika mashindano ya riadha ya dunia, kitengo cha mbio za masafa mafupi za 100m. Ndoto hiyo hata hivyo haikutimia.

Hii imempelekea Omanyala kufanya mabadiliko kadhaa katika mfumo wake wa maandalizi ikiwemo kumbadilisha kocha wake.

''Ilinibidi kufanya mabadiliko kwasababu nilitaka matokeo tofauti. Nimefanya kazi na huyu kocha wangu katika olimpiki zilizopita, na baada ya Olimpiki niliweza kukimbia kasi yangu ya kwanza chini ya sekunde 10, na kisha rekodi bora ya Afrika,'' Omanyala anasema. ''Nilitaka tuendelee kufanya kazi pamoja lakini kama ujuavyo kuna mengi yanayotokea hivyo nikaamua kufanya maamuzi kubadili kocha,'' anaelezea.

Chini ya Kocha wake mpya Omanyala analenga sasa mataji makubwa ya mwaka 2024 ikiwemo mashindano ya Dunia ya mbio za ndani mjini Galsgow- Machi 2024 na kisha Diamond league- July 2024.

''Awali nilikuwa nafanya kazi chini ya mwamvuli wa Shirikisho la Olimpiki Kenya. Lakini sasa mimi ni kocha wake moja kwa moja. Ina maana tutakuwa na muda zaidi pamoja kujitayarisha na kufiia malengo tuliyonayo,'' anasema Geoffrey Kimani, kocha mpya wa Omanyala.

Hata hivyo ili kuweza kuweka juhudi kamili katika malengo yake makuu ya mwakani, Omanyala na kocha wake wameamua kupotezea baadhi ya mashindano ikiwemo mashindano ya michezo ya bara Afrika (All African Games). Omanyala anasema kuwa watashiriki angalau mashindano thelathini zinazohitajika lakini zaidi atalenga mashindnao makubwa ya dunia ili kupata muda wa maandalizi.

Ferdinand Omanyala amebadilisha kocha wake kuendana n amalengo makubwa ya mwaka 2024 / Picha - Omanyala

Orodha ndefu ya mafanikio

''Katika miezi mitatu hii hatusafiri popote, na hatushiriki mashindano. huu ndio muda muafaka kufanya maandalizi. Tukianza mashindano kuanzia Februari hadi Septemba itakuwa hapa ki hapa,'' Omanyala anaambia TRT Afrika. ''

Omanyala ameibuka kama bingwa wa Kenya katika mbio za masafa mafupi, shindano ambalo halikuwa na uzoefu sana licha ya kuwa nchi hiyo ni vigogo katika riadha huku wanariadha wake tajika kama Faith Kipyegon, Eliud Kipchoge, Faith Cheruiyot, Kelvin Kiptum na wengineo wakivunja rekodi baada ya rekodi za dunia.

Miongoni mwa mataji alizojizolea Omanyala ni :

  • 3rd MoC Grand Prix, Yabatech Sports Complex, Lagos - 1st

  • The XXXII Olympic Games, National Stadium, Tokyo - 3rd

  • Int. JOSKO Laufmeeting, Pramtalstadion, Andorf - 1st

  • Kip Keino Classic, Moi International Sports Centre, Kasarani, Nairobi - 2 nd

  • 3rd Weekend Meeting, Nyayo National Stadium, Nairobi - 1st

  • ASA Athletics Grand Prix 4, Germiston Stadium, Johannesburg - 1st

  • Kip Keino Classic, Moi International Sports Centre, Kasarani, Nairobi - 1st

  • XXII Commonwealth Games, Alexander Stadium, Birmingham (SF2) - 1st

  • XXII Commonwealth Games, Alexander Stadium, Birmingham (F) - 1st

Ferdinand Omanyala alishinda mbio za 22 za Commonwealth Games, Alexander Stadium, Birmingham / Picha - Omanyala 

Licha ya kuwa mwanariadha anayejituma zaidi katika mazoezi na mashindno, Omanyala amerudisha shukrani zake kwa Mungu akisema kuwa imani yake ndiyo inayompa ujasiri wa kuendelea.

Kukuza vipaji zaidi

''Ninaamini kuwa Mungu ndiye chanzo kwa yote haya. Hii dunia tunapita tu kwa hiyo kitu cha muhimu ni kumtukuza Mungu kupitia kipaji alichokupa,'' anasema Omanyala.

Omanyala anakumbuka kuwa alipojitosa katika mbio hizi fupi, hakukuwa na ramani ya kufuata kwa Wakenya kwani haikuwa mazoea yao, lakini sasa vijana wengi chipukizi wanaweza kufuata mkondo wake.

'Natumai kuna siku itafika, ambapo tutakuwa na washindani zaidi ya mmoja wa mbio fupi Kenya. Sasa hivi wanapoita mshindani wa 100m, Omanyala, 200m Omanyala, sioni raha hapo. Sitaki kukaa peke yangu hapo juu,'' anaongezea Omanyala.

''Napenda sana nidhamu yake na mtazamo wake. sio mwoga na ana akili ya mshindi. Omanyala anacheka saa zote, hata ilinibidi nimtafute mke wake nimuulize ili nipate kumuelewa. Hata ukimbana katika mazoezi karibu azirai, utamuona anacheka tu, lazima umuelewe ili ujue kufanya kazi naye,'' anasema Kocha wake Kimani.

Ferdinand Omanyala anafanya kazi usiku na mchana kutimiza malengo yake ikiwa kushinda Olimpiki 2024 mjini Ufaransa/ Picha - Omanyala  

Vyovyote vile utakavyomtazama, Omanyala amekuwa jina tajik amiongoni mwa majina makuu nchini Kenya, Afrika na duniani. Anasema angefurahi kuweza kuvunja rekodi ya Usain Bolt siku moja ila anachukua hatua kwa hatua kwa sasa.

Japo amewatia moyo vijana wengi kujiunga na mbio fupi nchini Kenya, yeye bado analenga ndoto zake, na kufanyia kazi usiku na machana.

'Wakati nafanya mazoezi, najua kunao wanariadha wale walinishinda mbeleni, na sitaki wanishinde tena. Hilo ndilo lengo langu,'' anamalizia kusema omanyala.

TRT Afrika