Gyan, ambaye aliwahi kumaliza nafasi ya pili kwenye tuzo za Mchezaji Bora Afrika, CAF, mnamo 2010, ametoa tangazo hilo siku ya jumanne huku akiongeza kuwa atazidi kujihusisha na masuala ya kuinua vipaji vya mchezo huo barani.
Gyan alianza safari yake ya kusakata soka katika klabu ya Liberty Professionals akiwa na umri wa miaka 16, na kuishia kuvaa jezi za vilabu vya Al-Ain, Stade Rennais, Sunderland na Modena kabla ya kutundika ndaluga.
"Ningependa kuchukua fursa hii adhimu, kueleza hatua ambayo ni ngumu katika maisha ya kila mchezaji wa soka, muda ambao wanasoka wote hawataki lakini wakati asili inapopambazuka, sauti hiyo nyembamba itaendelea kujirudia masikioni mwao," alisema kwenye taarifa aliyoisaini.
Amezidi kuongeza, "Imefikia wakati, sauti hiyo imekuwa wazi masikioni mwangu, na nimekubali ni wakati wa kukabidhi jezi na buti kwa utukufu ninapostaafu rasmi kucheza soka," sehemu ya taarifa yake inasomeka.
Asamoah Gyan, ameuaga mchezo huo akiwa na sifa za ufungaji bora kutokana na uhodari wake mbele ya lango.
Mfungaji huyo maarufu ‘babyjet’ anashikilia rekodi ya mfungaji mwenye asili ya kiafrika mwenye magoli mengi katika kombe la dunia akiwa na magoli sita baada ya kushiriki kombe la dunia la 2006, 2010, na 2014.
Vilevile, baada ya kufunga goli lake la sita nchini Brazil mnamo 2014, alifanikiwa kumpiku Roger Milla wa Cameroon mwenye magoli matano.
Aidha, Gyan anashikilia rekodi ya kuwa mfungaji bora wa timu ya taifa ya soka ya Ghana, maarufu black stars, kwa kufunga magoli 51 kwenye mechi 109 na kufuta rekodi ya awali ya nyota wa zamani wa Ghana, Abedi Pele.
Vilevile, Gyan ni mchezaji wa kwanza mwenye asili ya Kiafrika kufunga katika Makala tatu tofauti ya kombe la dunia.
Licha ya ufanisi wake, hakufanikiwa kupokea medali ya Kombe la mataifa bora barani Afrika ingawa aliwahi kushiriki mashindano hayo mara saba ikiwa ni pamoja na kucheza fainali mara mbili.