Makala ya Kombe la tisa la Dunia la Wanawake litashuhudiwa bingwa wa mara ya kwanza baada ya washindi wote wa awali wa shindano hilo kuondolewa.
Hii ni baada ya 'Lionesses' wa England kutinga fainali yao ya kwanza ya Kombe la Dunia la Wanawake kwa kujinyakulia ushindi wa 1-3 dhidi ya Australia katika Uwanja wa Australia, Sydney / Wangal.
Ella Toone aliipatia England bao la uongozi kunako dakika ya 36 kabla ya Sam Kerr kuisawazishia Australia dakika ya 63.
Lauren Hemp alisukuma uongozi wa England mbele dakika ya 71 kabla ya Alessia Russo kufunga la tatu na la mwisho la 'Lionesses' dakika ya 86.
Baada ya washindi wa awali wa kombe la Dunia la Wanawake, Marekani, Ujerumani, Norway na Japan kuondolewa kwenye michuano hiyo nchini Australia na New Zealand, sasa Kombe hilo litakuwa na mmiliki mpya mwaka huu baada ya England na Uhispania kuweka historia kwa kutua fainali.
England itakutana na Uhispania kwenye fainali ya mashindano hayo yatakayofanyika kwenye Uwanja wa Australia huko Sydney/Wangal Agosti 20.
Uhispania ilijipa ushindi wa 2-1 dhidi ya Sweden kwenye mechi yake ya hatua ya nusu fainali.
Kwa mara ya kwanza katika historia, timu 32 zilichuana kuwania taji hilo baada ya kupanuliwa kutoka nchi 24 2015 kwenye makala yaliyopita huko Canada.