Familia ya Kelvin Kiptum imesema kuwa ndoto zao na matumaini yao ya baadaye yamevunjika kufuatia kifo cha Kelvin Kiptum kwenye ajali ya gari Jumapili usiku.
Kiptum na kocha wake kutoka Rwanda, Gervais Hakizimana, walifariki kwenye ajali hiyo karibu na mji wa Kaptagat magharibi mwa Kenya.
Eneo hilo liko katikati eneo la bonde la ufa, ambalo ni maarufu kwa kuzalisha wanariadha bora kutoka Kenya wanaong'ara kote ulimwenguni.
Baba wa Kiptum, Samson Cheruiyot ambaye anajishughulisha na kilimo amesema kwamba amepoteza mtoto wake wa pekee, mmoja ambaye alikuwa amemuahidi — siku moja kabla ya kifo chake — kumjengea nyumba na kumnunulia gari.
Kulingana na Cheruiyot, mama mzazi wa Kiptum alipatwa na matatizo wakati wa kumzaa mwanariadha hiyo, hali iliyomlazimu kutobeba ujauzito mwingine.
Mzee Cheruiyot bado anakumbuka mazungumzo ya mwisho na mwanaye yaliyofanyika Jumamosi usiku, ambapo Kiptum alimshirikisha utayari wake wa kushiriki mbio za Rotterdam Marathon zitazofanyika Aprili, huku akiazimia kumaliza mbio hizo kwa muda wa chini ya saa mbili hadi 1:58-1:59.
Kiptum alisitisha masomo yake katika uhandisi wa umeme na kugeukia riadha ambayo ilikuwa ni ndoto yake, Cheruiyot alisema.
"Alisema kwamba alikuwa na tajriba ya umeme ya kutosha, na kwamba ikiwa angeendelea kukimbia, angetuinua kiuchumi", baba yake akasema.
"Nilikubali na kwenda kumwandikia chumba karibu na kambi ya mazoezi ambapo alikaa hadi aliposhinda mbio zake za kwanza kubwa za marathon.”
Mkewe Kiptum, Asenath Cheruiyot, alisema walikuwa wasafiri pamoja Rotterdam mwezi Aprili, ambapo Kiptum alitarajia kumaliza mbio katika chini ya masaa mawili. Aliongeza kwamba Kiptum alipaswa kugharimia biashara zake.
"Wakati mwingine ningemwambia anafanya kazi sana," alisema. "Aliwapenda sana watoto wake, sijui nitawaambia nini.”