Na Lynne Wachira
TRT Afrika, Nairobi, Kenya
Bingwa wa dunia wa mbio za marathon Makala ya 2022 Tamirat Tola ndiye bingwa mpya wa mbio za mji mkuu wa New York, upande wa wanaume, ambazo zimekamilika Jumapili nchini marekani.
Tola alionyesha dalili za kushinda mbio hizo punde tu alipofika katika kilomita thelathini ambapo aliongeza kasi na kukiacha nyuma kikundi cha wanariadha wanne akiwemo bingwa wa mbio hizo Makala ya 2021 Albert Korir wa Kenya.
Juhudi zake zilizaa matunda matamu zaidi huku ushindi wake ukizidi kumaliza katika nafasi ya kwanza, kwa muda wa saa 2:04:58 ukidhibitishwa kuwa rekodi mpya ya mbio hizo za New York.
“Ninajivunia sana ushindi wangu wa leo haswa baada ya kupata maumivu ya tumbo wakati wa mashindano ya riadha ya dunia mjini Budapest na kulemewa kumaliza mbio hizo,” Tola alielezea furaha yake.
Ushindi wa Tola ulikuwa wa kipekee ikizingatiwa kuwa Albert Korir alimaliza mbio hizo katika nafasi ya pili dakika mbili baada ya Tola kutwaa ushindi.
Shura Kitata wa Ethiopia alimaliza katika nafasi ya tatu akitumia muda was aa 2:07:11.
Katika Upande wa wanawake , Hellen Obiri aliibuka mshindi kwa kutumia muda wa 2:27:23 huku akilazimika kukabiliana na upinzani usio kifani kutoka kwa mshikiliaji wa rekodi ya dunia ya mbio za mita elfu kumi Letesenbet Gidey wa Ethiopia.
Gidey aliridhika na nafasi ya pili kwa kutumia muda wa 2:27:29. Mbio hizo ziliwaleta pamoja wanariadha walio na uzoefu mkubwa akiwemo bingwa mtetezi Sharon Lokedi na aliyekuwa mshikialji wa rekodi ya dunia Bridgid Kosgei.
Wanariadha watano walisalia kwa pamoja pasiwe na kuongeza kasi hadi ilipofika kilomita 5 za mwisho ambapo Mkenya Viola lagat alitimuka ghafla na huku Obiri, Gidey na Lokedi wakifuata kwa karibu, walibadilishana uongozi hadi mita mia tano za mwisho pale Obiri na Gidey walijiondoa huku kila mmoja akionekana kuwa na kiu cha kuibuka mshindi.
Obiri alipata nafasi ya kulipiza kisasi baada ya kupoteza dhahabu ya mbio za mita elfu kumi kwa Gidey katika mashindano ya dunia mwaka uliopita.
“Nilifurahia sana jinsi mashabiki walilitaja jina langu na kunipa motisha nilipokuwa napita njiani, nilijiamini na kuamua kuwa mvumilivu na ndiposa sikukata tamaa licha ya upinzani mkali, kasi yake ya mbio za uwanjani ilikuwa nguzo mhimu sana katika ushindi wa leo.” alisema Obiri.
Obiri alihamia mbio za marathon mwaka uliopita na tayari amefanikiwa kushinda mbio za mji mkuu za Boston na mbio za New York Marathon.