Nyota wa Tanzania Mbwana Samatta na Miamba wa Ugiriki PAOK wako kifua mbele kwenye kinyang'anyiro cha kufuzu Europa Conference League baada ya kuwalaza Hearts 2-1 kwenye mechi yao ya mkondo wa kwanza iliyofanyika Tynecastle Park, Scotland, Alhamisi.
Hearts ya Scotland ilitumia faida ya kuwa mwenyeji na kuchukua uongozi mechini kupitia penalti iliyotiwa kimiani na nahodha Lawrence Shankland.
Hata hivyo, wageni PAOK wanaoongozwa na Razvan Lucescu, walitoka nyuma na kusawazisha mambo kuwa 1-1 dakika tatu baadaye kupitia penalti iliyopachikwa na Stefan Schwab baada ya Andrija Živkovic kuangushwa kwenye eneo la goli.
Baada ya kupokea pasi kupitia kiki ya kona, Andrija Zivkovic alipiga hatua kuelekea langoni na kuachia shuti kali kutoka nje ya eneo la hatari hadi kimiani na kumduwaza kipa Zander Clark, na kuipa PAOK ushindi muhimu dakika ya 75.
Mchuano huo ungekamilika sare ya 2-2 kabla goli la Lawrence Shankland kukataliwa na VAR kwa kuonekana kuwa ameotea.
Mbwana Samatta alikosa mechi hiyo kwani anaendelea kupokea matibabu baada ya kuumia kifundo cha mguu na goti katika mchezo wa awali wa PAOK dhidi ya Asteras mjini Toumba.