Mwanariadha bora wa kike duniani, na nyota wa mbio za mita 1500 Faith Kipyegon, huenda akaweka rekodi na kuwa mwanamke wa kwanza kukamilisha ushindi wa mara tatu mfululizo (hattrick) ya ubingwa wa taji la dunia la 1500m ikiwa ni pamoja na kuwa mwanamke wa kwanza kutimiza ubingwa huo mara mbili kwenye vitengo vya mita 1500 na 5000.
Faith Kipyegon atashiriki fainali za mbio ya mita 1500 upande wa wanawake kwenye Mashindano ya Riadha ya Dunia Budapest yatakayofanyika kwenye uwanja wa Kitaifa wa Riadha Hungary.
Hii ni baada ya kuwa mwanamke wa kwanza kuvunja kizuizi na kumaliza chini ya muda wa dakika 3:50 kwa 1500m, alipokimbia kwa muda wa 3:49.11 huko Florence, Italy mnamo Juni 2 na kuvunja rekodi ya maili huko Monaco mnamo 21 Julai.
Uhasimu wa Kenya na Ethiopia kwenye mbio pia unatarajiwa kwani, Kipyegon atashuhudia ushindani mkali kutoka bingwa wa wanariadha chipukizi Birke Haylom. Haylom mwenye umri wa miaka 17 ndiye alivunja rekodi ya dunia ya U20 ya Kipyegon nchini Poland.
Aidha, Mholanzi Sifan Hassan mwenye umri wa miaka 30 ambaye alifanikiwa kushinda mbio za mita 1500 na 10,000 mtawalia huko Doha nchini Qatar miaka minne iliyopita, na pia ambaye alishinda shaba kwenye mita 1500 kwenye Michezo ya Olimpiki ya Tokyo, pia anashiriki katika mbio hizo za 1500m.
Orodha hiyo inakamilishwa na wanariadha wengine wakiwemo Ciara Mageean, Jessica Hull, Katie Snowden, Cory Ann Mcgee, Laura Muir, Nelly Chepchirchir, Ludovica Cavalli, Melissa Courtney-Bryant, Na Diribe Welteji.