Amrabat punde tu baada ya kuzinduliwa rasmi. Picha: Manchester United

Kiungo wa kati wa Morocco Sofyan Amrabat, ametambulishwa rasmi kuwa mchezaji wa Manchester United baada ya kukamilisha taratibu za uhamisho na kukabidhiwa jezi nambari 4.

Sofyan Amrabat amejiunga na Manchester United kutoka ACF Fiorentina ya Italia kwa mkopo kusakata Old Trafford hadi Juni 2024.

"Ni heshima kubwa kuwa mchezaji wa Manchester United. Nimelazimika kuwa mvumilivu kwa wakati huu lakini mimi ni mtu ambaye husikiliza moyo wangu kila wakati na sasa ninawakilisha kilabu cha ndoto zangu.'' Sofian Amrabat alisema

Amrabat, ameiwakilisha Morocco mara 49 na na kujizolea sifa kutoka wapenzi wa soka kwa kukipiga kila dakika ya mechi za nchi yake Morocco na kuiwezesha kutinga nusu fainali ya Kombe la Dunia la FIFA la 2022 nchini Qatar.

Kocha Erik ten Hag ameeleza kwanini Manchester United wamemsajili Sofyan Amrabat na kile atakachochangia kwa timu hiyo.

"Anaweza kucheza pamoja na Casemiro kwa sababu pia anaweza kucheza sehemu ya juu kidogo uwanjani. Ana nguvu sana, ni mzuri sana katika mapambano. Kwa hivyo tunafurahi kuwa naye hapa United na nadhani atachangia malengo yetu ya juu tuliyoweka." Kocha Ten Hag alisema

Ni vizuri sana kuwa naye na nadhani anafaa sana kwenye Ligi Kuu ya Premier, na kwenye soka ya Ligi ya Mabingwa.

Ten Hag

Mbali na Amrabat, United pia ilifanya juhudi za mwisho kuimarisha kikosi chake kwa kuwasajili Kipa Altay Bayindir na walinzi Sergio Reguilon na Jonny Evans huku wakiinoa kikosi cha Erik ten Hag kwa msimu wake wa pili usukani.

Amrabat amelirithi jezi namba 4 kutoka kwa Phil Jones, ambaye aliihama klabu msimu huu wa kiangazi baada ya mkataba wake kuisha.

Mbali na Amrabat na Jones, wengine waliovaa jezi nambari 4 ni Owen Hargreaves, Juan Sebastian Veron, na Gabriel Heinze.

TRT Afrika